Saturday, August 29, 2015

👉Yohana 8:31-32 "Basi Yesu akawaambia wale wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli;  tena mtaifahamu KWELI, nayo hiyo KWELI itawaweka HURU".

👉Katika vizazi vyote, vita ya shetani ni kuhakikisha watu wote wanaangamia. Na vita kubwa inaelekezwa  kwa watu wanaomtafuta Mungu, Yesu Kristo alikuja kufunua hila zote za shetani ili atakayepotea awe ameamua mwenyewe. Kama ilivyokuwa wakati wa wayahudi, ndivyo ilivyo siku hizi, watu wengi wako katika mateka kwa mwamvuli wa DINI au UDHEHEBU. 
👉Katika Hosea 4:6, neno linasema "Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako". Shetani anazidi kutesa jamii, kwa Magonjwa, uchawi, mafarakano, ugonvi, chuki, kugombania madaraka, visasi, dhuluma kila kona, udanganyifu na utapeli, n.k. Ni wazi Bwana hayuko hapo.

👉Neno linasema, 2Timotheo 4:3-4 "Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia walimu makundi makundi, kwa kuwa wanamasikio ya utafiti, nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za UONGO". Tunaishi nyakati za kutimiza unabii huu, kama Yesu alivyotabiri juu ya manabii na makristo wanaochanganya ukweli na mapokeao yasiyo maagizo ya Mungu - Mathayo 7:15-23.

👉Neno la leo, linatoa ufunguo wa ufahamu, kwa watu wa kizazi hiki, waliozaliwa ndani ya makundi ya Dini na Madhehebu au ndani ya utitiri wa makundi ya Manabii na Mitume, chukua hatua ya dhati ya KUMUOMBA Mungu, ili afunue UKWELI WA NENO lake, kupitia mafundisho ya Yesu Kristo na uongozi wa Roho mtakatifu. Kumbuka UKWELI na UONGO au MAPOKEO hujitenga, wakati umefika kwa watoto wa Mungu kuwa HURU mbali na Mapokeo na kuuthibitisha wokovu wetu.

👉Wengi wanapofushwa hadi kuikataa Kweli kwa sababu ya roho za utambuzi na MIUJIZA, Yesu alitoa tahadhari - Mathayo 24:24-25 "Kwa maana watatokea makristo wa UONGO, na manabii wa UONGO, nao watatoa ISHARA kubwa na MAAJABU; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata WALIO WATEULE. Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele". Watu wengi wanakusanywa chini ya mwamvuli ya kujazwa roho na kupokea miujiza, kwa kutumia jina la Yesu na maneno baadhi ya biblia, lakini kwa ndani ni WAOVU, wafanya biashara, wazinifu, na udanganyifu mwingi kwa kwasiojua kweli, kwa nje wanaonekana ni Kondoo lakini kwa kipimo cha mbinguni ni waovu, mbwa mwitu wenye uchu, wakila kondoo zao.

👉Siku hizi, utasikia hawa ni watu wangu, hili ni kundi langu, usiliingilie, na wengine wanatishwa wakiambiwa usipotii sauti ya nabii utakufa au utalaaniwa, huku akiambiwa ameonyeshwa anatakiwa kumhudumia mtumishi kwa ngono, na mwanamke asiye mke wake. Kuna vituko vingi vinaendelea, na tunavishuhudia katika dini za leo. Kiongozi wa dini anafuga majini, wengine wanaenda kupata Upako kwa mizimu, halafu wanakuja kutisha watu na kuwagalagaza chini ya mavumbi eti ni nguvu ya roho  mtakatifu. Huo ni Ujinga wa kukosa maarifa, watu wanapofushwa macho kwa maneno laini ya kuwapa mibaraka, hawataki kuisikia Sheria ya Bwana inayokemea dhambi. Huo ni UHURU BANDIA.

👉Mpendwa, lithibitishe kila ulilofundishwa na unaloliamini kama ni agizo la Mungu au ni maagizo ya wanadamu. Uwe huru kutii neno la Mungu kuliko falsafa za wanadamu. Kila siku tunapaswa kukua kwa njia ya kujifunza neno la Mungu na kutakaswa, chini ya uongozi wa Roho mtakatifu. Udini na Udhehebu ni Kaburi refu litakalowaangamiza wengi tusipokubali kuwa HURU KATIKA KRISTO.

MUNGU AZIDI KUTUANGAZIA NURU YAKE - SIKU YA LEO IKAWE YA BARAKA TELE. 

Na: Ev Eliezer Mwangosi - Simu: 0767210299 - Email: eliezer.mwangosi@yahoo.com.
 
****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***
Categories:

0 comments:

Post a Comment

SIKILIZA NA DOWNLOAD WIMBO "KIFO" TOKA KWA PADACK

MAHUBIRI YA USHINDI HATIMAYE 2017 HAYA HAPA