Friday, September 16, 2016

Makamu Mwenyekiti wa Baraza kuu la Kanisa la Waadventista wa Sabato Ulimwenguni , Mchungaji Geoffrey Mbwana aliongoza zoezi la kuwasha mwenge katika viwanja vya kanisa la Burka SDA Arusha.

LENGO NI KUAMSHA NA KUHAMASISHA UENEZAJI WA INJILI KWA JAMII .
KITOVU KIKIWAWA NI KANISA LA BURKA-LILILOKO KATIKA JIMBO DOGO LA KASKAZINI MASHARIKI MWA TANZANIA.
Mnamo Mwaka 1904 wamishionari wa kwanza walifika Tanganyika wakitumwa na Konferensi ya Ujerumani kwa ajili ya kazi ya injili. Walifika Dar es Salaam mwezi wa Disemba na kuelekea milima ya Upare iliyoko Kaskazini Mashariki mwa Tanzania. Walifanikiwa kuanzisha kituo cha misheni katika bonde la Giti. Tangu Mwaka 1905 – 1912 vituo vya Kihurio, Suji na Gunta viliweza kuanzishwa ambapo waumini wa kwanza walikuwa wanane tu.
Mpaka kufikia mwaka 1950 injili ilikuwa imeenea maeneo mengi tofauti tofauti hapa nchini na Mwaka 1960 Makao Makuu ya Kanisa yalianzishwa huko Busegwe mkoani Mara na baadae kuhamishiwa Arusha eneo la Njiro kama Tanzania Union. 
Mnamo mwaka 2013 tarehe 4 Disemba iliyokuwa Tanzania Union ilitangazwa rasmi na mwenyekiti wa Kanisa la Waadventista wa Sabato Kanda ya Afrika Mashariki na Kati Mchungaji Blassious Ruguri kuwa na Union mbili ambazo ni Union Konferensi ya Kaskazini mwa Tanzania na Union Mision ya Kusini mwa Tanzania. Union Konferensi ya Kaskazini mwa Tanzania inajumuisha mikoa 13 ambayo ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Singida, Simiyu, Shyinyanga, Mara, Mwanza, Tabora, Kigoma, kagera na Geita. Union hii ina idadi ya makanisa 1929 yenye jumla ya washiriki 404,159.
Union Conference ya Kaskazini mwa Tanzania ina majimbo madogo 4, ambayo ni Mara Conference, South Nyanza Conference (SNC), West Tanzania Conference (WTC) na North East Tanzania Conference (NETC). Jimbo la NETC linajumuisha mikoa 4 ambayo ni Tanga, Kilimanjaro, Manyara na Arusha lenye jumla ya washiriki washiriki 67,216. Kanisa la Waadventista wa Sabato Burka linapatikana ndani ya Jimbo la Kaskazini Mashariki mwa Tanzania.
INJILI ARUSHA
Mnamo mwaka 1954 Eliamani Manase aliyekuwa muumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato alihamia katika Mkoa huu kikazi na ndiye aliyeanzisha injili katika Mkoa huu wa Arusha. Kwa juhudi zake binafsi alitafuta waumini wenzake wa kanisa hili na alifanikiwa kuwapata wachache ambapo walianzisha kundi la shule ya Sabato. Walikutana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukosa sehemu ya kuabudia, lakini Bwana ni Mwema kwani ilipofika mwaka 1961 walifanikiwa kupata eneo huko Sanawari wakiwa waumini 4 na wanafunzi 2. Baadae walipata eneo lingine huko Meru kwa mzee Ndelekwa Ikamba ambapo namba ya waumini iliendelea kuongezeka na kufikia watu 7. 
Mwaka 1962 familia ya Mama Yunis Natogolwa Kuga walihamia Arusha na bado hapakuwa na kanisa isipokuwa tawi hilo moja la Shule ya sabato. Washiriki hawa walifanya kazi ya uinjilisti katika mazingira magumu kwani kulikuwa na kanisa moja tu na watu walikuwa wakitembea mwendo mrefu kwenda kanisani lakini pia kutawanya vijizuu na masomo ya Sauti ya Unabii. Katika mwaka huo waliendesha effort ya kwanza ya nyumba kwa nyumba iliyoendeshwa na Mchungaji Bender maeneo ya Sanawari na watu wasiopungua 10 walibatizwa. 
BURKA KUPATIKANA
Mnamo mwaka 1967 jengo la kanisa la Burka lilinunuliwa toka kwa makaburu wa Afrika ya Kusini. Washiriki wakiwa na mchungaji Bender walifurahi sana na kumshukuru Mungu kwa kupata nyumba ya ibada. Waliendelea kufanya kazi ya uinjilisti kwa bidii japo katika mazingira magumu kwani walikuwa wakitembea kwa miguu mwendo mrefu lakini Bwana aliwawezesha na idadi ya waumini iliongezeka.
Sabato ya kwanza kusali katika kanisa hili alieongoza ibada alikuwa Mchungaji Cril Bender na Mashemasi walikuwa Upendo Yoel, Yunis Natogolwa Kuga, William Senkoro na Eliamani Manase, Mtunza Kanisa wa kwanza alikuwa Mbonea Kiondo ambaye pia alikuwa Mkuu wa Kundi hilo la Burka. Mwinjilisti wa kwanza wa Vitabu alikuwa ni Elibariki Misheto aliyetumwa kutoka Field. Mwaka 1964 familia ya John Mhina iliongezeka.
Siku za pasaka walikuwa wakisali huko Majengo Moshi na hiyo ilikuwa kila Sabato ya kwanza ya kila Mwezi. Mwaka 1965 Ubatizo ulifanyika na aliyebatiza alikuwa Mchungaji Yohana Lusingu, waumini waliobatizwa ni familia ya Mzee Ndelekwa, Upendo Yoel, Jotham Lukwaro na Daud Obayo.
Mwaka 1966 ulifanyika mkutano mkubwa kwa miezi sita, mikutano hiyo ilifanyika katika eneo la Hosptali ya Kaloleni. Waliobatizwa katika mkutano huo ni: Nairoki Lotanywaki na kijana wake Nsinyari na binti zake wawili. Mchungaji wa kwanza alikuwa Tumaini Abraham ambaye alikufa kwa kuumwa na nyuki, baadae alifuata Mchungaji Uze Kajiru baada ya Mtumishi wa Bwana kulala mauti.
Makundi ya kwanza kutoka Burka yalikuwa ni: Tengeru, Monduli, Kijenge likifuatiwa na kundi lililokuwa likisali katika Shule ya Msingi Meru, Kundi la Unga Limited lilikuwa likisali katika Shule ya Msingi Sinoni. Mtaa wa kwanza kutengwa toka Burka ulikuwa ni Mtaa wa Meru ikifuatiwa na Mtaa wa Njiro na Sanawari.
Kanisa hili limechungwa na Wachungaji wafuatao:
Mch. Tumaini Abraham
Mch. Uze Kajiru
Mch. Daniel Nahato
Mch. Anderson Fue
Mch. Joseph Namfua
Mch. Samwel Panga
Mch. Elisante Mkiramwene
Mch. Elias Peter Lomai
Mch.John Wilfred Kimbute
Mch. Isaya Kanana
Kwa sasa Kanisa hili linachungwa na Mchungaji Simon Mnyindo akisaidiana na Wazee wa Kanisa Zephania Malima, Daud Charles, Steven Katengu na Elia Nyeura. Mashemasi ni Bennett Msovu na Catherine Buyabara pamoja na Wahazini Simeon Matiko, Helen Mong’ateko na Sitty Gamba.
Kanisa hili linayo kwaya ya Kanisa iliyosajiliwa rasmi mwaka1986 ikiwa na wanakwaya 40 chini ya mwenyekiti na Mwalimu Lazaro Jonas akisaidiana na waalimu Joshua Otuoro na Malaki Saka (ambaye kwa sasa ni Marehemu). 
Mpaka sasa Kwaya imefanikiwa kutoa matoleo 24 ya Audio na 4 ya DVD. Kwaya hii kwa kwa mwaka huu wa 2016 imefanikiwa kusajili wanakwaya wapatao 80 na walimu ni Aloyce Mabula, Zadock Otieno, Joshua Otuoro, Samwel Ongiri, jerry Kairanya na Lameck Chacha.
Kwa neema ya Bwana Kanisa la Burka limeendelea kufanya kazi ya utume kwa bidii na limefanikiwa kuongeza idadi kubwa ya washiriki na hivyo kuweza kuwa na mitaa 12 na makanisa takriban 50 yenye jumla ya washiriki 20,013 kati ya hao washiriki 736 wanatoka kanisa la Burka. Kanisa pia limefanikiwa kupeleka injili maeneo ya umasaini na kuweza kujenga makanisa maeneo ya Lovilukunyi, Ngaramtoni ya Chini, Olchorovus, Matevesi na Engorora. Kanisa pia limefanikiwa kununua vyombo vya sauti.
Kwa sababu idadi ya washiriki inaongezeka Kanisa linao mpango wa muda mrefu kuwa na Jengo kubwa la ibada ili kuikidhi mahitaji ya kanisa. Lakini pia kuna mpango wa muda mrefu wa kuwa na kituo cha mvuto (Center of Influence) Pamoja na nyumba ya Mchungaji. Kanisa limeanza mpango huo wa ujenzi na washiriki wameshirikishwa kwa kuanza kuchangia vifaa mbalimbali vya ujenzi.

MOTTO: BURKA 2016 - ONDOKA UANGAZE, YESU ANAKUJA


Habari/Picha na Abel Kinyongo


****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***
Categories:

1 comment:

  1. Amani mwakalindile, mbona huna aibu? hoja ya Mashauri Mafuru ni kimaandiko, unapaswa kumuonyesha kimaandiko, acha maneno ya mudomoni, hayo kila mtu anayo, lakini swala la Mwenge kwenye bilia Isaya {50:11}, imekataza mwenge,Mungu amekataza. mara jeshi, sasa mwenge, mh!? mmefika mbali. Mtamsurubisha Kristo mara ya pili hata lini?

    ReplyDelete

SIKILIZA NA DOWNLOAD WIMBO "KIFO" TOKA KWA PADACK

MAHUBIRI YA USHINDI HATIMAYE 2017 HAYA HAPA