Ev. Eliezer Mwangosi.
Isaya 43:18-19 "Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua Sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji Nyikani".
Wapendwa, tukiwa tumebakiza masaa machache kuufunga mwaka 2014 na kuuanza mwaka mpya 2015, Ambao kwa mujibu wa NENO la Mungu utaanza jioni ya tarehe 31, kila mtu ana jambo la kusema juu ya aliyoyapitia kwa mwaka mzima wa 2014. Wengine ulikuwa ni mwaka wa mafanikio, mambo kwa ujumla yalikuwa tambalale, wakati wengine wamepitia changamoto zenye Machungu makubwa, huku wengine wakiona miaka yote ni sawa tu hawana jipya. Bila kujali ulipitia au uko katika hali Gani! Leo nina habari njema kwako, Mungu atafanya jambo jipya katika Maisha yako.
Inawezekana umepitia au bado uko ndani ya changamoto za maisha, hali ya uchumi ni mbaya, maisha yanapanda huku vipato vinazidi kuwa....
na kwashakoo (haviongezeki), huenda ni Ada ya chuo au shule inakukosesha usingizi. Je ni mahusiano ya uchumba au ndoa yaliyo kuumiza?, wengine hata sikukuu ya Krismasi haikusaidia, walitegemea Yesu azaliwe ndani ya mioyo ya wanaume na wanawake, ndio kwanza walimsulubisha Yesu kwa dhambi ya Zinaa na ulevi, ndoa nyingi zimejeruhiwa na kujaa Machungu badala ya Raha, kila kunapokucha huzuni zinaongezeka katika Familia - Bwana anayatazama hayo na atafanya jambo JIPYA.
Je ni madeni ambayo kila ukiwaza namna ya kuyalipa unakosa majibu na kuanza kuwakwepa wanaokudai?, Je ni mikosi na balaa inayokuandama, kila ukijaribu biashara inaishia kukata mtaji, ukijaribu kilimo mvua hazinyeshi, ukifanikiwa kuvuna soko linakuwa shida. Je ni kuonewa kazini? hakuna anayethamini kazi yako, wengine wananyanyaswa lakini hawana jinsi, wanafanya kazi ili mradi kumekucha.
Je mapito yako ni Ugonjwa ambao umekata tamaa kuwa hauna tiba?, Je ni Upweke wa kuishi bila kuolewa au kuoa kwa kukosa Wachumba waaminifu? Na wakati wote unakutana na matapeli wa mapenzi wanaopenda kuonja na kutimua wanapoambiwa kuhalalisha?. Je ni kukosa ajira, umetembea na bahasha za maombi na vyeti hadi zinachanika, bila kujali viwango vizuri vya Kufaulu?, Changamoto yako huenda ni kupata watoto, uko katika ndoa ambayo imegeuka uchungu kwa kutokuzaa, unachukiwa na ndugu huku ukibezwa kila kona. Je ni tabia za watoto kuwa Mbaya? wamesombwa na mafuriko ya ulimwengu ya kuvaa milegezo, kulamba unga, kulala nje ingawa kwa Kutoroka, wanakataa kusoma shule, ni watu wa kujirusha n.k.
Haijalishi umepitia au bado uko ndani ya changamoto fulani, kupitia ujumbe huu, kwa Imani, kuna JAMBO JIPYA litaenda kutendeka kwako katika mwaka wa 2015 sawasawa na Ahadi za Bwana. Huyu Mungu aliyeumba ulimwengu kwa kutamka, anafanya njia pasipo njia kama alivyofanya njia katikati ya Bahari Waisraeli wakapita, Ndivyo atakavyofanya kuliondoa tatizo lako.
Na wale ambao mwaka 2014 ulikuwa wa kutesa kwa zamu, wakiwa ndani ya mafanikio na Raha mstarehe, wasije wakasahau Kumshukuru Mungu na kufanya agano upya na Mungu ili apate kuwalinda, maisha bila Mungu ni kujilisha UPEPO, ni kitendo cha kufumba na kufumbua, mtu anaingia kwenye huzuni kama si mauti ya Aibu. Jiulize je hayo mafanikio ya maisha yana dhambi ndani yake? Kama Jibu ni ndiyo! Usijidanganye SHETANI AMEKUTIA KITANZI SHINGONI unasubiri amri ya Kunyongwa kwa muda usioujua hata kama ni miaka kadhaa baadaye, hatima yake ni Aibu.
Nawatakia wote Baraka tele kwa mwaka 2015, sawasawa na ahadi za Bwana.
Ev. Eliezer Mwangosi.
Eliezer.mwangosi@yahoo.com
Tel. 0767210299
****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0789 243 413 NA 0717 367 693***




0 comments:
Post a Comment