Na Elizabeth Edward, Mwananchi
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu amesema kuchelewa kwa
uandikishwaji na utoaji wa vitambulisho hivyo katika mikoa mingi hapa
nchini kumesababishwa na uhaba wa fedha na rasilimali watu.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la
Wafanyakazi wa Nida, alisema kuwa licha ya mamlaka hiyo kuendelea na
shughuli zake, lakini inakabiliwa na changamoto ya rasilimali fedha na
rasilimali watu hali inayozoretesha utendaji na mikakati ya kuendelea na
usajili katika mikoa ya Tanzania.
“Mpaka sasa Nida imepiga hatua kubwa katika
Usajili na Utambuzi wa watu na ugawaji wa Vitambulisho vya Tafa, lakini
bado tunakabiliwa na changamoto ya rasilimali fedha na watu hali
inayochangia kuzorotesha utendaji,” alisema Maimu.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi Pereira Ame Silima, ameitaka Nida kuhakikisha changamoto
zinazojitokeza kutafutiwa ufumbuzi ili Watanzania wote wenye sifa waweze
kupata haki ya msingi ya kikatiba ya kusajiliwa na kupata vitambulisho.
Silima alisema kuwa Serikali itaendelea kusaidia
mamlaka hiyo ili kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya nne ya kila
Mtanzania kusajiliwa na kupata kitambulisho.
“Serikali kupitia Wizara yangu tutaendelea
kuongezea nguvu na mamlaka kufikia malengo iliyojiwekea. Lengo ni
kuhakikisha tunafanikiwa na Watanzania wote wanapata
vitambulisho,”alisema Silima.
Silima alisema Nida ina wajibu na dhamana katika
usalama wa nchi kama zilivyo taasisi nyingine, hivyo hawana budi
kuhakikisha mradi huo unatekelezeka na wananchi ambao idadi kubwa ni
masikini wananufaika ipasavyo.
SOURCE,MWANANCHI
****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***
0 comments:
Post a Comment