Mkuu wa majeshi nchini Burundi Meja
Jenerali Prime Niyongabo ametoa wito kwa wanasiasa kutotumia jeshi la
taifa kwa manufaa yao ya kisiasa.
Jenerali Niyongabo amekariri
tangazo lililotolewa na waziri wa ulinzi Jumamosi kuwa jeshi la nchi
hiyo litahakikisha kuwa mkataba wa Arusha umetekelezwa kikamilifu na
kuwa jeshi hilo halitumiwi na mtu au chama chochote cha kisiasa.Kuhusiana na maandamano yanayoendelea, mkuu huyo wa jeshi amesema kuwa maandamano hayo sio halali na wanaichi wanapaswa kutumia mbinu za sheria zilizopo kutatua mizozo yao.
Wakati huo huo Meja Jenerali Niyongabo amesema jeshi hilo litasalia kuwa lenye nidhamu ya hali ya juu na tiifu kwa taifa la Burundi na wala sio kwa mwanasiasa yeyote.
Ameongeza kusema kufikia sasa jeshi limefanya kazi nzuri kuhakikisha kuwepo kwa usalama nchini Burundi na katika mataifa mengine wanakohudumu katika vikosi vya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika.
Huku hayo yakijitokeza muungano wa upinzani umesema kuwa maandamano yataendelea siku ya Jumatatu baada ya mapunziko ya siku mbili.
Upinzani umepinga hatua ya rais Pierre Nkurunziza ya kuwania muhula wa tatu kama rais.
Viongozi wa upinzani wanasema kuwa Rais Nkurunziza ni sharti atekeleze mkataba wa Arusha ambao ulimaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi.
Lakini chama tawala cha CNDD FDD kimepinga madai hayo na kusema kuwa Rais Nkurunziza anatumikia muhula wake wa kwanza kwa sababu, miaka mitano ya kwanza ilikuwa kipindi cha mpito na hakuchaguliwa na raia kama inavyohitajika kisheria.
Idadi kubwa ya raia wa Burundi wamekimbilia nchi jirani kwa hofu ya kuzuka mapigano zaidi. Habari na BBC Swahili
****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***
0 comments:
Post a Comment