Monday, December 14, 2015

Tazama,  nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. Ufunuo 3:20.

1⃣ Yesu  asema, "Tazama, nasimama mlangoni, nabisha." Je! tutamfungulia? Yeye asingependa kutuona sisi tukisimama wakati huu, katikati ya hatari kubwa za siku za mwisho, kwa nguvu zetu wenyewe za kibinadamu.... Ni haki yetu kutembea katika mwanga wa jua wa kuwapo kwake, na kufuma katika tabia zetu tunazozijenga kamba zile za dhahabu za uchangamfu, shukrani, uvumilivu, na upendo. Kwa njia hiyo tunaweza kuonyesha uwezo wa neema ya Mungu, na kuakisi [kuiangaza] nuru ile itokayo mbinguni katikati ya wasiwasi na maudhi yanayotujia siku kwa siku.... Basi, mbona tunatembea kwa kujikwaa katika njia yetu bila kuwa na nuru hiyo?

2⃣Kila  onyo, kila karipio, na kila ombi katika Neno la Mungu, au kupitia kwa wajumbe wake aliowatuma, ni kubisha [kugonga] mlangoni pa moyo wako; ni sauti yake Yesu, ikiomba kuingia ndani yako. Kila bisho [kugonga] unalolidharau, huifanya azma yako ya kutaka kufungua kufifia zaidi na zaidi. Kama sauti hiyo ya Yesu haisikilizwi mara moja, basi, itachanganyika pamoja na sauti zingine nyingi katika moyo wako, yaani, masumbufu ya dunia na shughuli zake, mambo hayo yatachota mawazo yako yote, na hisia hiyo [ya kusikia sauti ya Yesu] itatoweka [moyoni mwako]. Moyo wako utaguswa kidogo tu, na kuishia katika hali ile ya hatari ya kupoteza uwezo wake wa kutambua hata usiweze kujua ufupi wa wakati ulio nao, na umilele ulioko ng'ambo ile ya pili.

3⃣ Wengi  wanazo takataka nyingi sana walizozilundika mlangoni pa moyo wao hata hawawezi  kumruhusu Yesu kuingia ndani. Wengine wana matatizo kati yao na ndugu zao ambayo hayana budi kuondolew [kusuluhishwa], wengine wana hasira mbaya, kiburi, uchoyo; kwa wengine ni kule kuipenda dunia kunakoweka kizuizi mlangoni pao. Vyote hivyo ni lazima viondolewe, kabla hawajaweza kufungua mlango na kumkaribisha ndani Mwokozi wao. 

4⃣Ni ya thamani jinsi gani ahadi hii, "nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami." Lo! ni pendo lililoje, pendo la ajabu la Mungu kwetu sisi! Baada ya sisi kuwa na uvuguvugu wote huu na dhambi tulizo nazo, yeye anatuambia, Nirudieni, nami itawarudieni, nami nitawaponya na kurudi nyuma kwenu kote.

5⃣  Kazi  yetu sisi ni kuufungua mlango wa moyo wetu na kumkaribisha Yesu ndani. Anabisha [Anagonga] akitaka kuingia ndani yako.... Je! utaufungua mlango? Yesu anasimama nje ya mlango wa moyo wako. Mkaribishe ndani, Mgeni wako huyo wa mbinguni.

NEEMA YA MUNGU WETU IKATAWALE MAISHANI MWETU DAIMA - NAWATAKIA SIKU NJEMA



****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***
Categories:

0 comments:

Post a Comment

SIKILIZA NA DOWNLOAD WIMBO "KIFO" TOKA KWA PADACK

MAHUBIRI YA USHINDI HATIMAYE 2017 HAYA HAPA