Sunday, January 01, 2017

Tafakari: Yohana 8:31 "Basi Yesu akawaambia wale wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli, tena mtaifahamu kweli; nayo hiyo kweli itawaweka huru."

Miaka kadhaa iliyopita, kulikuwa na kijana mmoja ambaye alikuwa kibaka, yaani mwizi wa mitaani, mara kadhaa alikuwa anapelekwa mahabusu, lakini jambo la ajabu akitolewa anarudia tena kuiba. Baadaye ikaja kugundulika kuwa, anapenda kukaa mahabusu au rumande, kwa sababu pale analala na kula japo ni mahali pabaya kwa kuishi.

Kuna lugha isemayo, za mwizi arobaini, aliporudia kuiba, zikatimia, wananchi wakamkamata na kuamua kumchoma moto hadi mauti. Kuna wengi wameizoea dhambi, japo kwa mionekano yao ni kama wacha Mungu, wakishinda na vitabu vya dini bila kukosa Misa au Ibada na wengine wakifanya kazi ya Mungu hadi ya kuimba, huku wakidumu kuwa watumwa wa dhambi.

Vitendo vya chuki, hila, unafiki, umbea, masengenyo, kutopendana, kutakiana mabaya, kulipa baya kwa baya na visasi, wivu, kutunga uongo, mafarakano, ubinafsi, kujiona, kujikwenza na kupenda sifa, kuingilia ndoa na kuvuruga mahusiano ya wengine, kujiunza, vitendo vya ngono nje ya ndoa, ulevi, wizi na  kupenda kuhongwa n.k. ni tabia za kawaida hata kwa wanaojiita wacha Mungu.

Wito wa Yesu katika tafakari ya leo, ni wote kutoka katika vifungo hivyo vya shetani na kuwekwa huru kabla siku hazijatimia, mazoea hujenga tabia, na uovu huo ukizoeleka inakuwa ni tabia ya mtu. Ni wakati wa kila mmoja kuchukua hatua ya kuishi sawasawa na neno la kweli la Kristo, peke yetu hatuwezi, bali tukimwamini Yesu Kristo na kuruhusu atawale maisha yetu, ushindi ni hakika.

NAWATAKIA SIKU NJEMA YENYE BARAKA TELE.

Na:  Ev Eliezer Mwangosi
Simu: 0766 210 299 na WhatsApp: 0766 992 265
.

****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***

0 comments:

Post a Comment

SIKILIZA NA DOWNLOAD WIMBO "KIFO" TOKA KWA PADACK

MAHUBIRI YA USHINDI HATIMAYE 2017 HAYA HAPA