Zekaria 9:9 Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda.
Yesu anawapenda waishio mijini na kwenye majiji. Yeye alitumia muda wake mwingi wa miaka 33 aliyoishi hapa duniani kuwahudumia watu wa mijini na kwenye majiji. Taarifa yake ya kazi iliyoandikwa na mwinjilisti Yohana inasema “Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.” Mathayo 9:35.
Aliupenda mji wa Yerusalemu hadi akaulilia. “Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.” Luka 19:41-44
Wakati huu tena Yesu analitembelea jiji la Dar es Salaam. Haji akionekana kama alivyokuja wakati wa uhai wake. Anakuja akiwatumia watumishi wake ambao wamejawa na huruma kama zake. Watumishi hao wanakuja na habari njema ya wokovu. Wakiwaandaa watu wa Dar es Salaam kwa tukio kuu litakalokuwa na furaha kuu kwa wakazi wote. Wanakuja kuijulisha Dar es Salaam kuwa mfalme wao anakuja. Wanakuja kuichangamsha Dar kwa nyimbo. Wanakuja kuichangamsha Dar kwa mahubiri yenye matumaini, wanakuja kuijaza Dar na kitabu cha Tumaini, wanakuja kuiponya Dar kwa kuipatia suluhisho la magonjwa. Wanakuja kuiponya Dar kwa kuipatia suluhisho la migogoro ya ndoa. Wanakuja kuiponya Dar kwa kuipatia suluhisho la matatizo ya kiuchumi. Wanakuja kuiponya Dar kwa kuipatia mahubiri yenye matumaini. Wanakuja kuiambia Dar “changamka mfalme wako anakuja.”
Utakuwa wakati wa kujulishwa cha kufanya ili kujiokoa na hatari inayoinyemelea Dar es Salaam. Utakuwa pia ni wakati wa kuililia Dar kwa kuipa maonyo yenye upendo. Utakuwa wakati wa kufahamu upendo wa Mungu ulivyotutoa kwenye kifungo cha dhambi. Utakuwa wakati wa kufahamu upendo wa Mungu utakavyotupa ujasiri siku ya hukumu. Utakuwa wakati wa kufahamu upendo wa Mungu unavyotubidisha kumtii. Utakuwa wakati wa kufahamu upendo wa Mungu unavyotupa ushindi dhidi ya dhambi. Utakuwa wakati ambao utabaki katika kumbukumbu zetu kwa muda mrefu ujao
Mahubiri haya yenye uvuvio yatasikika kwa mfululizo wa majuma matatu kuanzia tarehe 1 hadi 21 Juni mwaka huu kutokea Redio yako uipendayo ya Morning Star na kusikika kote nchini Tanzania na nje ya mipaka ya Nchi. Mahubiri hayo yatakuwa yakitolewa na mtumishi wa Mungu mchungaji Magulilo Mwakalonge. Mchungaji huyu anao ujumbe unaotoka kwa Mungu ambao hupaswi kuukosa. Kando ya mahubiri hayo yatakayokuwa yakirushwa kutoka kituo cha redio kilicho Mikocheni, kutakuwa na mahubiri mengine yatakayokuwa yakirushwa katika kipindi hicho hicho katika vituo takribani 123 vilivyo katika jiji la Dar es Salaam na viunga vyake. Huhitajiki kwenda umbali mrefu kuyafuata mahubiri haya. Tumejitahidi kuyaleta haya jirni na wewe ili unufaike na mambo mengi yaliyotayarishwa. Usikose kuhudhuria. Usikose kuwaalika marafiki zako, majirani zako, ndugu zako na wote uwapendao. Katika kila kituo kutakuwa na huduma za mafunzo ya afya na huduma ya afya ya msingi. Kutakuwa na mafunzo ya ndoa na familia. Kutakuwa na huduma ya Nyimbo za injili kutoka vikundi mbalimbali. Kutakuwa na huduma ya mahubiri yenye uchambuzi wa kina wa Neno la Mungu. Kutakuwa na huduma za ukarabati mdogo mdogo wa vifaa mbalimbali kulingana na mahitaji. Waendeshaji wa mikutano hii ambao ni Waadventista wa Sabato watahusika kufanya huduma kusafisha mazingira, kutembelea vituo vya yatima, na mahospitalini kwa ajili ya uchangiaji wa damu n.k. KARIBU UJIUNGE NA WENGI WANAOPANGA KUHUDHURIA MIKUTANO HII.
*** TUMA PICHA NA HABARI KWA WATSUP SASA NO 0717-367 693***



0 comments:
Post a Comment