Sunday, September 21, 2014

HATUA YA KWANZA"KUTAMANI"-NA TAMAA YAKE MWENYEWE
Kwa kusema kila mtu hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe unafikiri Yakobo ana maana gani? Mimi namuele anasema kila jaribu lina chanzo na chanzo chake ni tamaa ya mwanadamu. Samsoni asingeangushwa na Delila kama asingemuwakia tamaa delila. Yule rafiki asingeweza kukushawishi kama usingekuwa na hamu naye. Ile pesa isingekutia majaribuni kama usingekuwa na hamu nayo. Unaweza kusema kama Hawa lakini fulani alinianza. Hapana hakuna tena mjadala wa kuku na yai nani alianza. Mjadala umekwisha fungwa kwa maneno ya mtume, kila mtu hujaribiwa kwa tamaa yake mwenyewe. Tamaa inayokuchemka haichemkii nje bali ndani yako mwenyewe.

Unapohisi msukumo wa kutazama maungo yake, kuisikia sauti yake, au kunusa harufu yake tambua msukumo hautoki nje bali ndani yako. Kama uchu wa kutaka haupo nafsini mwako hata jaribu likuite kwa nguvu kiasi gani hautashtuka. Huko moyoni ndiko zitokako chemichemi za tamaa. 

Kama moyo wako ni safi basi utabubujisha tamaa safi. Kupitia macho ya moyo uliotakata utamuona Mungu popote, hata mahali asipotazamiwa. Badala ya kumtazama mwanamke uliyekutana naye kisimani kama mtego wa kukuangusha, utamuona kama binti wa Mungu anayehitaji kuheshimiwa na kuokolewa. Lakini kama moyo wako umejaa uchu wa fisi utatenda sawa sawa na hazina ya moyo wako. Paulo aliliweka jambo hilo vizuri aliposema, “vitu vyote ni safi kwa hao walio safi; lakini hakuna kilicho safi kwao walio wanajisi, wasioamini; bali akili zao zimekuwa najisi, na nia zao pia.” (Tit 1:15). Ukweli ndiyo huu, kimwingiacho mtu hakimtii mtu unajisi ila kimtokacho—na kimtokacho mtu, Yakobo anasema, ni tamaa yake mwenyewe.

Lakini Yakobo amemaliza kusema? Hajazungumzia upande mmoja tu wa sarafu katika kuainisha chanzo cha jaribu? Hapana—Yakobo amemaliza. Kama huamini, hebu leo serikali ipige marufuku nguo fupi uone kama hutatamani tena. Hebu kimbilia jangwani ukaishi huko pekee yako—pasipo na wanadamu wa kukukwaza—uone kama hutakwazika. 

Vikwazo au vishawishi sio chanzo cha majaribu. Kudhani ukiwa na pesa za kukutosha ndiyo unaweza kumrudishia Mungu  ni kujidanganya. Kudhani kama mpenzi wako akijirekebisha hutavutiwa na wengine ni kujihurumia bure. Yule secretary ofisini, ile chupa mezani au ule ukurasa mtandaoni siyo mchawi wako. Hapana, hapana. Ukweli wote ndiyo huu—tamaa yako mwenyewe ndiyo inayokuloga. 

Ole wangu mimi kijana niliyelogwa! Nifanye nini na mwili huu wa tamaa? Pole, nakuelewa rafiki. Hata mimi mguuni nina kiatu kama chako. Lakini tusijiurumie kupita kiasi. Mwenzako sikumsikia Yakobo akisema tamaa tulizonazo ni dhambi. Aa Aa! Hawezi kusema hivyo. Yakobo anajua ni tabia ya Bwana kuwapatia wanawe zawadi njema na si vipaji vibaya (1:16). Mungu wa mianga aliyetundika taa angani habadiliki. Mungu ana msimamo kuliko jua, mwezi, na nyota zinazo hama hama angani kwa utaratibu wa siku na majira (1:17). Haiwezekani jana awe amekupatiaa mwili wenye hisia halafu leo aseme tamaa ni dhambi.

Kumbuka ni Mungu ndiye aliyekuwekea mate mdomoni na mihehemuko damuni. Ni Yeye anayefyatua warembo kila kukicha (wanasema, wazuri hawajazaliwa). Ni Yeye aliyekupa macho yenye kuvutiwa na urembo. Tamaa ulizonazo mwilini ndizo alizopewa Yesu katika ubinadamu wake. Yesu hakuwa na mwili wa plastiki: alihisi hamu ya kuwa na rafiki, kula, kupumzika sawa sawa na sisi. Tamaa kama tulivyozipokea toka mikononi mwa Muumba hazina ubaya. Ninajua, kazi ya Mungu haina makosa. 

Lakini mabadiliko yanakujaje? Iweje tamaa njema uliyopewa kuifurahia igeuke kuwa tamaa mbaya ya kuijutia? Kisu ni kile kile ila kinaweza kukatia mboga au kuchoma watu. Tamaa ni ile ile ila malengo yake hubadilika. Kwanza, tamaa inapokuchochea utimize matakwa yake kinyume na sauti ya Mungu ndipo inakuwa tamaa mbaya. Unapojisikia upite njia ya mkato badala ya kuzunguka kwa kufanya kazi halali na kwa bidii ili upate—elewa hiyo ni tamaa mbaya. 

Pili, tamaa inapokuamsha uitimizie madai yake zaidi kuliko ulivyoruhusiwa na Mungu ndipo tamaa safi hugeuka kuwa tamaa chafu. Ni halali kulamba ice cream wakati fulani. Lakini hamu ikikushurutisha ulambe hata daktari akikuambia mwili wako hauihitaji tena tamaa ya ice cream inageuka haramu. Labda niseme, unapochagua kufurahia tamaa yako binafsi kinyume au zaidi ya atakavyo Mungu ndipo tamaa hugeuka kuwa dhambi.. Kabla tamaa haijakufikisha dhambini tamaa si dhambi.



Ni Bwana pekee, “awezaye ku[ku]linda [wewe] [u]sijikwae, na ku[ku}simamisha mbele ya utukufu wake bila mawaa katika furaha kuu” (Yud 24). Lakini ili uweze kufaidi ushindi wake, Mungu anataka ujue mapema mitego ya  adui wako. Utamshindaje adui usiyemfahamu? Katika pambano la wema na ubaya hakuna ushindi wa kubahatisha. Ushindi wa hakika ni matokeo ya ushirikiano mzuri baina ya Mungu na mwanadamu. Unapojua mapema mkakati wa kivita wa adui yako ndipo utaweza kuzitumia sila zote za Mungu kujihami na kumshambulia adui. 

Adui anatumia utaratibu upi wa kutushambulia na majaribu? Mungu alijua tutauliza swali hilo. Ndiyo maana akamuongoza mtume Yakobo atueleze majaribu hutufikia kwa hatua zipi kabla hayajatuletea maafa. Kwa maneno machache mtume anasema, “Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa [kunaswa]. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.” (Yakobo 1:14-15). 

Yakobo anatuambia, kabla ya kufikwa na mauti, muumini anajaribiwa hatua kwa hatua—huku hatua moja ikiita hatua nyingine. Kama ulimsikiliza vizuri uliona mchakato mzima una hatua saba. Hebu tuchunguze mkakati mzima. Kwa vipi unamtoa mlengwa toka kwenye usalama kwenda kwenye hatari. Uchunguzi huu utatufumbua macho tuuone mstari mwekundu mapema na kuchukua tahadhari badala ya kuuvuka pasipo kujua na kuangamia. Sasa hatua ya kwanza ni ipi?





















****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***

0 comments:

Post a Comment

SIKILIZA NA DOWNLOAD WIMBO "KIFO" TOKA KWA PADACK

MAHUBIRI YA USHINDI HATIMAYE 2017 HAYA HAPA