![]() |
| Punje ya haradani |
Siku moja ya wiki iliyopita nilibahatika kushuhudia imani kidogo kama punje ikizaa matokeo makubwa. Tulikuwa tumetoka tu kumaliza mahubiri ya injili ya jioni hiyo. Nilipokuwa nikiaga wanatimu wenzangu walinijia na ripoti, "mchungaji, tumekutana na mama mmoja si mbali na hapa kanisani ambaye anayekuhitaji ukamfanyie huduma." Nilihisi hii ni kesi nzito. Hapo nyuma, tulikubaliana kwamba mimi na wao tulipewa mamlaka sawa Yesu alipotutuma kazini. Wanaweza kuwaombea wagonjwa au kutoa pepo pasipokuniita. Iweje sasa niitwe?
Nilipohoji umuhimu wa mimi kuongozana nao kwa huduma walinijibu, "pastor, sisi tulimwambia tungeweza kumhudumia. Lakini mama huyo alikataa na kusema niitieni mchungaji wenu." Upesi nikaelewa wanatimu wangu wana imani kubwa ila mwanamke waliyekutana naye ndiye mwenye imani haba. Basi, tukakubaliana kesho yake saa kumi jioni twende tukamtembelee.
Muda tuliokubaliana ulipofika mimi na akina mama watatu tukafika katika mji mmojawapo wa Ubungo Kibangu, Dar es Salaam. Kutuona, Mama akafurahi na kusema, "ndiyo huyu mchungaji wenu?" Wakamjibu, "ndiyo mwenyewe." Moyoni nikasema laiti kama mama huyu angelitambua mimi ni mwanadamu tu.
Bila kupoteza muda mama akaanza kunisimulia kisa na mkasa. Akaniambia wameshindwa kulala kwa siku kadhaa. Nyumba yao haina amani tangu wakutane na chungu kikiwa kimefukiwa mbele ya mlango wa nyumba yao na mtu wasiomfahamu. Nikamuuliza, "chungu chenyewe kiko wapi?"
Mama akanionesha kwa kunyosha mkono wake, huku uso wake ukionesha hofu. Nilipojaribu kuangalia, nikaona kweli mdomo wa chungu ukichungulia huku kiwiliwili chake kikiwa kimefukiwa ardhini. Nikamgeukia na kumuuliza, "kwa hiyo unataka msaada gani?" Akanijibu, "naomba unifukulie na unitupie mbali balaa hili." Nilijua mama amechoka na anataka amani.
Ndipo nilipomfungulia Biblia na kumweleza kwa maneno machache namna ya kupata amani ya ya uhakika na ya kudumu. Kisha nikawakusanya wanatimu wenzangu na tukaomba. Baada ya hapo nikaagiza vifaa vya kufukulia. Akaniletea jembe na zoleo. Nikachimba na kuchimba. Mama macho yote kwenye chungu. Nilipomaliza kufukua, kweli tukaona ni chungu cheusi na ndani yake konokono mweupe! Mama mwenyewe akawa makini kwamba sibakizi chochote hapo. Sikumuangusha. Uchafu wote nikaukusanya na kuutupia katika korongo nje ya nyumba yake. Baada ya kumuaga kwa ombi tulimwacha hapo akiwa na furaha na sisi kurudi mkutanoni.
Siku mbili baadaye, wanatimu wenzangu walirudi kwa yule mama kumjua hali. Yule mama akasema,"tangu siku mliyokuja tumeweza kulala kwa amani. Hapo nyuma tulikuwa tunasikia miguu inatembea juu ya dali, mara tukabwe, kila usiku mahangaiko matupu tukisubiri kupambazuke. Lakini sasa tunalala bila usumbufu wowote."
Ushuhuda huo ukanikumbusha ukweli wa maneno ya Yesu aliposema, “Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.” (Mathayo 17:20). Niliona udogo wa imani yake aliposisitiza mchungaji tu na si wainjilisti akamsaidie kupambana na nguvu za giza. Aliamini bila kuona shaka kwamba Mungu asingemuangusha mchungaji.
Mwanamke wa Kibangu amenifundisha si ukubwa wa mbegu bali ubora wake ndiyo unaohitajika kwa matokeo makubwa sasa. Nilidhani Mungu alinitumba Dar kuwafundisha watu wa Ubungo imani. Kumbe Mungu alinituma mimi huko ili wana Ubungo wanifundishe imani. Sasa simuombi Bwana aniongezee imani bali aniboreshee imani. Nataka imani bora na si bora imani.
BOFYA HAPA KWA MASOMO MENGINE ZIDI****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***




0 comments:
Post a Comment