Sehemu
ya Ghala la kuhifadhi vitunguu Saumu liliojengwa na MIVARF, lipo Mkoani
Manyara Wilayani Mbulu, kijijini Bashay. Ghala hilo lina uwezo wa
kuhifadhi tani 50 za vitunguu Saumu.
Na. Ibrahim Hamidu
Programu
ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha
Vijijini (MIVARF) imeboresha Soko la Vitunguu Saumu kwa kujenga ghala la
kuhifadhi vitunguu mkoani Manyara, wilayani Mbulu katika kijiji cha
Bashay.
Ghala
hilo lenye uwezo wa kuhifadhi tani 50 za vitunguu, limegharimu Jumla ya
shilingi milioni 88 ikiwa MIVARF imechangia asilimia 95 ya fedha hizo na
Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imechangia asilimia 5 ya fedha hizo.
Akiongea
na timu ya wataalam kutoka MIVARF ofisini kwake hivi karibuni wakati
timu hiyo ilipokuwa ikikagua utekelezaji wa shughuli za Mradi huo, Kaimu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Bw. Nicholaus Haraba,
alifafanua kuwa ujenzi wa ghala hilo umeongeza mnyororo wa thamani wa
zao la vitunguu Wilayani Mbulu.
“Tunaushukuru
Mradi wa MIVRAF kwa ujenzi wa ghala hili la kuhifadhi vitunguu ambalo
ni ghala pekee kwa hapa nchini lenye viwango sitahiki na uwezo wa
kuhifadhi tani nyingi za vitunguu. Kwa mantiki hiyo ghala hili
limewawezesha wakulima wa zao hilo kuongeza thamani ya mazao yao ambayo
awali yalikuwa yanapotelea shambani kwa kukosa eneo la kuyahifadhi ”
alisema Haraba.
Haraba
alieleza kuwa, kupitia MIVRAF wananchi wa Mbulu wamepata mafunzo ya
jinsi ya kufungasha mazao yao pamoja na kuwezeshwa vifungashio vya
vitunguu hali ambayo imelijengea ubora zao hilo katika soko.
“Wananchi
awali walikuwa wanauza mazao yao huko mashambani, katika mabeseni na
lumbesa lakini baada ya mafunzo ya MIVARF ya jinsi ya uhifadhi wa mazao
yao hivi sasa wananchi wanauza vitunguu kwa vipimo kwa kutumia
vifungashio maalum hii inamfanya mkulima kunufaika na mauzo hayo”
alisisitiza Haraba.
Aliongeza
kuwa, katika kuhakikisha Soko la Vitunguu linakuwa imara Wilayani
Mbulu, MIVARF imejenga barabara kwa kiwango cha Changarawe kutoka
Bashay, Diyomat, Dirima hadi Muslur yenye Urefu wa km 25 kwa gharama ya
shilingi milioni 789 ikiwa asilimia 95 ya fedha zilizotolewa na MIVRAF
na asilimia 5 zimetoka katika Halmashauri ya Mbulu.
“Ujenzi
wa barabara hii pia utasaidia kwa wafanyabiashara kusafirisha kwa
usalama mazao hayo baada ya kuyanunua kutoka Mbulu” alisisitiza Haraba
Katika kuunga juhudi za MIVARF za kuboresha Soko la Vitunguu tayari
Halmashauri ya Wilayani Mbulu katika bajeti yake ya mwaka 2015/2016
imetenga kiasi cha shilingi milioni 18 kwa ajili ya ununuzi wa mashine
ya kusindika vitunguu ili wafanyabiashara wanunue vitunguu ambavyo
tayari vimesindikwa na tayari kumuuzia mtumiaji wa mazao hayo.
“Tunategemea
MIVARF iendelee kuliboresha soko hili la vitunguu na jukumu letu
nikuchangia kwa kile tunachowezeshwa na MIVARF hivyo tumeamua kutenga
fedha katika bajeti ya mwaka ujao ili tutakapowezeshwa kununua mashine
ya kusindika vitunguu tuwe tayari kwa ajili ya ununuzi wa mashine yetu”
alisema Haraba.
Akiongea
na Wataalamu wa MIVRAF katika ghala la kuhifadhi Vitunguu la Bashay
Wilayani Mbulu, Mkulima wa zao hilo, Bi. Wema Edward alibainisha kuwa
Mradi wa MIVRAF umeliboresha soko la vitunguu wilayani humo kwa kuongeza
mnyororo wa thamani wa zao hilo.
“Kutokana
na uhifadhi bora wa vitunguu na vifungashio bora hivi sasa tunauza kilo
ya vitunguu kati ya shilingi elfu 3,000/= hadi elfu 4, 000/= , wakati
awali tulipokuwa tunatumia mabeseni kuhifadhi mazao yetu tulikuwa
tunauza kilo kwa shilingi elfu 1,500/=. ” alisema Wema. Mradi wa MIVRAF
ambao unahudumia wananchi 4,800 wilayani Mbulu ulianza kutekelezwa
katika wilaya hiyo kuanzia mwaka 2013, katika kata tatu za Wilaya hiyo,
kwa kuongeza thamani mazao na ujenzi wa miundo mbinu ya masoko.
Programu
ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha
Vijijini (MIVARF) ni Programu iliyobuniwa na Serikali Tanzania
ikishirikana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Benki
ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani Afrika
(AGRA). Programu hii ni ya miaka saba inayotekelezwa katika mikoa yote
ya Tanzania Bara na Zanzibar. Utekelezaji wake ulianza rasmi mwezi Julai
2011.
****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***

.jpg)


0 comments:
Post a Comment