Yohana
8:31-32 "Basi Yesu akawaambia wale wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa
katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu
KWELI, nayo hiyo KWELI itawaweka HURU".
Katika
vizazi vyote, vita ya shetani ni kuhakikisha watu wote wanaangamia. Na
vita kubwa inaelekezwa kwa watu wanaomtafuta Mungu, Yesu Kristo alikuja
kufunua hila zote za shetani ili atakayepotea awe ameamua mwenyewe.
Kama ilivyokuwa wakati wa wayahudi, ndivyo ilivyo siku hizi, watu wengi
wako katika mateka kwa mwamvuli wa DINI au UDHEHEBU.
Katika
Hosea 4:6, neno linasema "Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa;
kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe
kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami
nitawasahau watoto wako". Shetani anazidi kutesa jamii, kwa Magonjwa,
uchawi, mafarakano, ugonvi, chuki, kugombania madaraka, visasi, dhuluma
kila kona, udanganyifu na utapeli, n.k. Ni wazi Bwana hayuko hapo.
Neno
linasema, 2Timotheo 4:3-4 "Maana utakuja wakati watakapoyakataa
mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia
walimu makundi makundi, kwa kuwa wanamasikio ya utafiti, nao
watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za UONGO".
Tunaishi nyakati za kutimiza unabii huu, kama Yesu alivyotabiri juu ya
manabii na makristo wanaochanganya ukweli na mapokeao yasiyo maagizo ya
Mungu - Mathayo 7:15-23.
Neno
la leo, linatoa ufunguo wa ufahamu, kwa watu wa kizazi hiki,
waliozaliwa ndani ya makundi ya Dini na Madhehebu au ndani ya utitiri wa
makundi ya Manabii na Mitume, chukua hatua ya dhati ya KUMUOMBA Mungu,
ili afunue UKWELI WA NENO lake, kupitia mafundisho ya Yesu Kristo na
uongozi wa Roho mtakatifu. Kumbuka UKWELI na UONGO au MAPOKEO hujitenga,
wakati umefika kwa watoto wa Mungu kuwa HURU mbali na Mapokeo na
kuuthibitisha wokovu wetu.
Wengi
wanapofushwa hadi kuikataa Kweli kwa sababu ya roho za utambuzi na
MIUJIZA, Yesu alitoa tahadhari - Mathayo 24:24-25 "Kwa maana watatokea
makristo wa UONGO, na manabii wa UONGO, nao watatoa ISHARA kubwa na
MAAJABU; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata WALIO WATEULE. Tazama,
nimekwisha kuwaonya mbele". Watu wengi wanakusanywa chini ya mwamvuli ya
kujazwa roho na kupokea miujiza, kwa kutumia jina la Yesu na maneno
baadhi ya biblia, lakini kwa ndani ni WAOVU, wafanya biashara, wazinifu,
na udanganyifu mwingi kwa kwasiojua kweli, kwa nje wanaonekana ni
Kondoo lakini kwa kipimo cha mbinguni ni waovu, mbwa mwitu wenye uchu,
wakila kondoo zao.
Siku
hizi, utasikia hawa ni watu wangu, hili ni kundi langu, usiliingilie,
na wengine wanatishwa wakiambiwa usipotii sauti ya nabii utakufa au
utalaaniwa, huku akiambiwa ameonyeshwa anatakiwa kumhudumia mtumishi kwa
ngono, na mwanamke asiye mke wake. Kuna vituko vingi vinaendelea, na
tunavishuhudia katika dini za leo. Kiongozi wa dini anafuga majini,
wengine wanaenda kupata Upako kwa mizimu, halafu wanakuja kutisha watu
na kuwagalagaza chini ya mavumbi eti ni nguvu ya roho mtakatifu. Huo ni
Ujinga wa kukosa maarifa, watu wanapofushwa macho kwa maneno laini ya
kuwapa mibaraka, hawataki kuisikia Sheria ya Bwana inayokemea dhambi.
Huo ni UHURU BANDIA.
Mpendwa,
lithibitishe kila ulilofundishwa na unaloliamini kama ni agizo la Mungu
au ni maagizo ya wanadamu. Uwe huru kutii neno la Mungu kuliko falsafa
za wanadamu. Kila siku tunapaswa kukua kwa njia ya kujifunza neno la
Mungu na kutakaswa, chini ya uongozi wa Roho mtakatifu. Udini na
Udhehebu ni Kaburi refu litakalowaangamiza wengi tusipokubali kuwa HURU
KATIKA KRISTO.
MUNGU AZIDI KUTUANGAZIA NURU YAKE - SIKU YA LEO IKAWE YA BARAKA TELE. Na: Ev Eliezer Mwangosi - Simu: 0767210299 - Email:
eliezer.mwangosi@yahoo.com.
****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***
0 comments:
Post a Comment