Wednesday, September 02, 2015

 👉Waebrania 12:14-15 "Tafuteni kwa bidii kuwa na AMANI na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemuona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie NEEMA ya Mungu; shina la UCHUNGU lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo".

👉Kila ninapojaribu kufuatilia mijadala mbalimbali juu ya kampeni zinazoendelea, nakutana na maneno ya mipasho, jazba, na wakati mwingine matusi. Kama watumishi wa Mungu, tuna wajibu wa kuisaidia jamii kufikia malengo yao katika uchaguzi kwa AMANI na UHURU. Huu ni wakati wa kuomba, badala ya kupoteza muda mwingi kubishana kwa maneno ya malumbano na ushabiki.

👉Tukumbuke kuwa serikali au vyama vya SIASA havina Dini, hivyo kupata AMANI ya kweli katika mashindano ya kisiasa bila Mungu ni ndoto, watu wa Mungu ndio pekee wanaweza kuleta AMANI ya Kweli na ya kudumu katika jamii kwa Uweza wa Mungu. Ninaamini wote tunapenda mabadiliko yenye tija, hakuna anayependa umaskini au dhuruma na adha mbalimbali tunazozipata kijamii, swali la msingi ni hili; tutafikaje salama katika hitaji letu?

👉Kumbuka, ni Mungu pekee mwenye jibu sahihi asilimia 100, ndiye anayejua ajenda za siri za nyuma ya pazia za wagombea, pamoja na sera nzuri zinazotolewa kutoka kwa vyama, bado tunapaswa kuwa na uhuru wa kumwendea Mungu kwa maombi ili atupatie kiongozi atakayetimiza ndoto zetu. Narudia, ni Mungu pekee mwenye mamlaka na MAAMUZI ya mwisho ya kumuweka kiongozi atakayewafaa watu wake, tusipomhusisha Mungu; na tukaamuwa wote tutumie misukumo ya hisia zetu, Mungu atatuacha tuchague, ila mwisho tutakiona, kama waisraeli walivyolilia awapatie mfalme kinyume na matakwa ya Mungu wakaambulia majuto.

👉Hebu watoto wa NURU; tuamke tumwambie Mungu atupatie Kiongozi atakayetufaa. Katika vizazi vyote Mungu ndiye mwenye maamuzi ya mwisho, hapo hakuna kuiba kura, wala nguvu ya mafuriko, yeye akisema laa ni laa, akisema ndio ni ndio. Soma - Warumi 13:1 "Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na iliyopo imeamriwa na Mungu". Mamlaka yoyote iwe nzuri au mbaya, imeruhusiwa kwa wakati huo kwa makusudi fulani. Watu wa Mungu ndio wenye wajibu wa kuongea na Mungu atupatie anayefaa, kwani hakuna hila wala mbinu za kibinadamu zinazoweza kumshinda Mungu, yeye ndiye mwenye maamuzi ya Mwisho.

👉Ushauri kwa wagombea na walioko madarakani: Mungu anajua kama ahadi zinazotolewa ni za kweli au viinimacho, watu wamechoka, wanahitaji mabadiliko ya kweli, sio ya kutapeliwa na kuingizwa katika hali mbaya kuliko mwanzo. Mungu anajua ni nani aliye mkweli, na aliye na uwezo wa kukidhi hitaji la watanzania katika AMANI ya kweli itakayodumu. Kumbukeni; wanyenyekevu na wacha Mungu watainuliwa, na waongo, wenye hila na kujitukuza; Bwana atawaangusha kwa mkono wake usioonekana.

👉Rejea watawala wa dunia waliojiinua na kusema hakuna wa kuwashinda, kwa majivuno hayo, walitolewa kwenye mamlaka, kwa mkono wa Mungu - Danieli 4:24-32 (Mfalme wa babeli, Nebukadreza alitolewa kwenye mamlaka na kupelekwa msituni akaishi kama mnyama). Danieli 5:17-31, (Mfalme wa babeli Belshaza, aliuwawa na jeshi dogo la Dario kwa agizo la Mungu, baada ya kumdharau Mungu mwenye mamlaka).

👉Mwisho: Mbali na upenzi au ushabiki wa vyama, bado watu wa Mungu tunapaswa kumuomba Mungu atupatie Kiongozi anayemuona ATAFAA kwa ajili ya utukufu wake, sio kama sisi tupendavyo, kwa hisia zetu za kibinadamu, zisizojua yaliyoko mbele. Kila mtu awe huru kupiga Kura yake ili kutimiza hitaji la demokrasia chini ya uongozi wa Mungu, bila kushurutishwa kwa namna yoyote. Mwenye hekima Sulemani alisema - Mithali 18:18 "KURA HUKOMESHA MASHINDANO; HUKATA MANENO YA WAKUU".

👉Nawatakia wote neema ya Mungu iwapatie moyo wa kuwapenda wanaowaudhi na kuwaombea, na moyo wa jazba, harara na matusi visionekane kwenu, ili shina la uchungu lisije likachipuka ndani yenu na kuwafanya WAOVU mbele za Bwana.

AMANI YA BWANA IPITAYO AKILI ZOTE IKATAWALE SASA NA HATA MILELE.

 ***** Ukiona vema, Wapelekee wengine ujumbe huu ********

Na: Ev. Eliezer Mwangosi - Simu: 0767210299 - Email: Eliezer.mwangosi@yahoo.com.

****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***
Categories:

0 comments:

Post a Comment

SIKILIZA NA DOWNLOAD WIMBO "KIFO" TOKA KWA PADACK

MAHUBIRI YA USHINDI HATIMAYE 2017 HAYA HAPA