Monday, January 18, 2016

Tafakari: Yakobo 4:13-16 "Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi. Lakini sasa mwajisifu katika majivuno yenu; kujisifu kote kwa namna hii ni kubaya".

Wahenga walisema hujafa hujaumbika, ni jambo la kawaida katika kizazi chetu kuona akina dada na akina kaka wakijitahidi kubadiri sura au maumbile, wakitafuta urembo, mara zote mioyo imejaa mahangaiko ikitafuta uzuri, na hatimaye mioyo inajaa majivuno, kujiona na kuwadharau wengine.

Jambo la hatari zaidi, taratibu lakini kwa uhakika mioyo yao inatiwa giza na kujitenga na Mungu, huku wakikuza tabia ya kujipenda nafsi na kuipenda dunia kuliko kumpenda Mungu. Wengi wamenaswa na mitindo ya dunia, wakijitahidi sana kuhudhuria majumba ya Ibada, lakini mioyo ikiwa mbali na utii wa neno la Mungu.

Mungu anawauliza akisema "Uhai au Uzima wenu ni Nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo kisha hutoweka". Pamoja na mipango mingi ya kujiongeza na maisha haya, Mungu ndiye mwenye maamuzi ya mwisho juu uhai wetu. Uzuri wote, na madaha yote pamoja mipango mingi, bila Mungu ni kujilisha upepo.

Ukitaka kujua kuwa ni NEEMA YA MUNGU TU uko hivyo, tembelea hospitali, uone warembo wanavyosaidiwa na mashine kupumua, kashuhudie wengine wakiwa wametafunwa na saratani, wengine wakiwa wamepooza, na wengine wakiwa wamepoteza viungo kwa ajali n.k. Hebu kila mmoja ajiulize, ana nini cha zaidi Mungu amempatia afya njema?

Kiburi kinatoka wapi wakati hata pumzi tunayopumua ni kwa neema ya Mungu? Je ya kesho nani anayajua kama si Mungu, hivi Mungu akisahau kurudisha ufahamu tunapokuwa tumelala usingizi usiku itakuwaje? Mungu anauliza tena "UZIMA WAKO WEWE MWANADAMU NI NINI BILA MUNGU?".

Mwenye hekima atafakari neno la leo na kuamua kufanya matengenezo, mpingeni shetani, mtiini Mungu, kwa maana maisha bila Kristo katika uhai huu, ni HASARA YA MILELE.

NAWATAKIA SIKU NJEMA YENYE KUJAA BARAKA ZA BWANA.

Na. Ev. Eliezer Mwangosi -  Simu: 0767 210 299.


****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***
Categories:

0 comments:

Post a Comment

SIKILIZA NA DOWNLOAD WIMBO "KIFO" TOKA KWA PADACK

MAHUBIRI YA USHINDI HATIMAYE 2017 HAYA HAPA