Sunday, June 12, 2016

Yesu ni jibu la changamoto yoyote inayokutokea inayohusu uzima wa milele au chochote kinachokutatiza. Marko 10:17-21 “Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele. Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako. Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.” Njia moja ya kujua usahihi wa jambo lolote lenye utata ni kumwuliza Yesu. Hata unapokabiliwa na maamuzi magumu na hujui nini uamue jiulize Yesu angekuwa kwenye nafasi yako angefanyeje. Na kama bado hupati majibu bado unatakiwa umwendee Yesu katika maombi. Mathayo 6:6 “Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.”
Itafuteni haki ya Mungu
Kijana tajiri katika kisa hiki anawakilisha Wayahudi wa wakati wa Yesu waliokuwa waaminifu kwa utunzaji wa amri lakini wakakosa kukifikia kiini cha sheria yenyewe. Warumi 9:31-33 “Bali Israeli wakiifuata sheria ya haki hawakuifikilia ile sheria. Kwa sababu gani? Kwa sababu hawakuifuata kwa njia ya imani, bali kana kwamba kwa njia ya matendo. Wakajikwaa juu ya jiwe lile likwazalo, kama ilivyoandikwa, Tazama, naweka katika Sayuni jiwe likwazalo, na mwamba uangushao; Na kila amwaminiye hatatahayarika.” Warumi 10:3 “Kwa maana, wakiwa hawaijui haki ya Mungu, na wakitaka kuithibitisha haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu. Kijana tajiri alipungukiwa na haki ya Mungu ipatikanayo kwa imani katika mkombozi Yesu Kristo. Chochote unachofanya bila Yesu ni bure. Yesu ni kila kitu, Yesu ni jibu, na Yesu anatosha.

Utii unaotokana na shukurani
Hatutunzi amri za Mungu ili tuokolewe, bali tunatunza amri kwa kuwa tumeokolewa. Yohana 14:15 “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.”Ni namna ya kuonesha shukrani zetu kwa aliyetuumba na kutukomboa. Waisraeli walipewa Amri baada ya kuokolewa. Kutoka 20:2-3 “Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu mingine ila mimi.” Wale wanaotunza sheria wakifikiri itawasaidia kuibua huruma za Mungu au kuwastahilisha kuokolewa wanakosea sana. Warumi 3:20 “Kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.” Lakini sheria imewekwa pale ituelekeze kile tunachopaswa kufanya kwa msaada wa Mungu. Yenyewe ingawa haijapewa uwezo wa kuokoa ni kitu kizuri kabisa. 1 Timotheo 1:8 “Lakini twajua ya kuwa sheria ni njema, kama mtu akiitumia kwa njia iliyo halali.” Warumi 7:12 “Basi torati ni takatifu, na ile amri ni takatifu, na ya haki, na njema.” Sheria inawakilisha tabia ya Mungu ambayo tuliipoteza tulipoanguka dhambini tabia ambayo Mungu anatamani tuirudie. Waefeso 2:8-10 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.

Sisi ni mavumbi
Tuliumbwa tutende matendo mema lakini dhambi ilitia udhaifu miilini mwetu tukawa tumepoteza kabisa uwezo huo. Kile Mungu anachotuagiza kufanya hatuwezi kukifanya kwa uwezo wetu wenyewe. Yohana 15:5 “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.” Tabia tunayoonesha kwa nje ni ile inayotokana na tulivyo ndani. Mathayo 12:34 “Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake.” Mungu hatarajii wanadamu watende mema ambayo hawana uwezo wa kuyazalisha. Yeremia 13:23 “Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya.” Mungu hatukatishi tamaa ya kutenda mema bali anatujulisha ugumu wa jambo lenyewe. Ule wema tunaojaribu kufanya bila msaada wa Mungu huishia kuwa kitu cha kuchukiza. Isaya 64:6 “Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo.”

Mungu na ufumbuzi wa tatizo letu
Shida yetu ni ya Mungu pia. Yeye amefanya njia pasipo na njia. Ametujalia uwezo wa Roho Mtakatifu ili atusaidie kurekebisha tabia zetu zilizopinda. Hatua ya kwanza Roho anayofanya ni kutushuhudia kuwa tumetenda dhambi. Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?” Matendo 5:33 “Wao waliposikia wakachomwa mioyo yao; wakafanya shauri kuwaua.” Matendo 7:54 “Basi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno.” Unaposikia moyo unachoma kwa ujumbe mkali unaotoka kwa Mungu hiyo ni kazi ya Roho Mtakatifu.

Kuficha dhambi
Dhambi inapofunuliwa huleta maumivu. Lakini ujanja siyo kuwa mbishi bali ujanja ni kutoa ushirikiano. Mithali 28:13 “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.” Dhambi inapofunuliwa huleta aibu na ndiyo maana wengine huamua kutotoa ushirikiano. Lakini wale wanaokuwa wanyenyekevu wakati dhambi yao inapofunuliwa hupata faida kubwa zaidi ya kusamehewa. Warumi 4:7-8 “Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao. Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi.” Matendo 3:19 “Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana.” Hatua ya kwanza muhimu katika kushinda dhambi ni kutoa ushirikiano na Roho Mtakatifu anapotufunulia mapungufu yetu ya kiroho tukitambua kuwa hakuna binadamu aliye mkamilifu na ya kuwa pasipo Yesu sisi hatuwezi neno lolote. Mungu akubariki unapotafakari hayo.



****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***
Categories:

0 comments:

Post a Comment

SIKILIZA NA DOWNLOAD WIMBO "KIFO" TOKA KWA PADACK

MAHUBIRI YA USHINDI HATIMAYE 2017 HAYA HAPA