Saturday, July 02, 2016

Hatua ya mwisho katika kuhitimisha pamabno kuu lililodumu kwa miaka 6,000 ni kurithi ufalme. Wanadamu wanaorithi ufalme wanarithishwa kile ambacho hawakustahili. Hawarithishwi kwa sababu ya uwezo wao wa kutii yaliyoagizwa bali kwa utayari wao wa kuamini kile wanachoagizwa na walichoahidiwa. Ni urithi ulioahidiwa na Mungu tangu zamani. Mathayo 25:34 “Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu.”
Urithi ni tamko linalotolewa na mzazi kwa mwanae au kwa mtu yeyote aliyemchagua kuwa atanufaika na utajiri alionao baada ya kufa kwake. Urithi ni tofauti na mkataba kwa sababu katika mkataba pande mbili hukubaliana kutimiza wajibu fulani kwa upande wa pili ili kustahili kunufaika na kile kinachoahidiwa na upande mwingine wa mkataba. Kama wanadamu wangeingia mkataba na Mungu ikawapasa wanadamu kwa upande wao kufanya jambo fulani la kustahili kupewa uzima wa milele. Maandiko yanatuambia kuwa uzima wa milele unamhusu mtu mmoja. Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”
Ili Uzima wa Milele upatikane, mwanadamu anatakiwa kuamini. Kwa hesabu za haraka haraka inaweza kuonekana kuwa mwanadamu ananunua uzima wa milele kwa kuonesha imani kwa Yesu. Lakini Biblia hiyo hiyo inakanusha dai hilo. Yohana 6:44 “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho.” Hata mitume walitambua kuwa hawana ujanja wa kujizalishia imani ambayo ni ya muhimu sana ili waokolewe. Luka 17:5 “Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee imani.” Yesu anahusika si katika kutuongezea imani tu, bali ndiye anayetuanzishia imani hiyo pia. Waebrania 12:2 “Tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.” Hata kama umepata uzima wa milele kwa kumwamini Yesu hiyo imani si yako ni mali ya Mungu kwa hiyo huna cha kujisifia ni neema ya Mungu tu. Waefeso 2:8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.”
Uzima wa milele umelinganishwa na mtu aliyefanya karamu ambapo baadhi ya walioalikwa hawakunufaika nayo kwa sababu ama walikataa kuja ama waliokubali walikataa kufuata maelekezo ya mwenye karamu. Kwa siku zilizopita tumekuwa tukishughulikia umuhimu wa kukubali mwaliko huu kuzingatia maelekezo ya mwenye karamu. Kutozingatia maelekezo ya mwenye karamu hakuishii kwa kutolewa karamuni bali kunaandamana na kuadhibiwa. Mathayo 22:8-13 “Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili. Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini. Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni. Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi. Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa. Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.” Mungu ameandaa karamu nyingine kama hiyo amabyo sote tumealikwa. Ufunuo 19:9 “Naye akaniambia, Andika, Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo. Akaniambia, Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu.”
Mwaliko huu ulianza kwa Abrahamu. Kumbukumbu 7:7-8 “Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako; Bwana Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi. Bali kwa sababu Bwana anawapenda, na kwa sababu alitaka kuutimiza uapo wake aliowaapia baba zenu, ndiyo sababu Bwana akawatoa kwa mkono wa nguvu, akawakomboa katika nyumba ya utumwa, katika mkono wa Farao, mfalme wa Misri.”
Moja ya matatizo makubwa mtoto mkaidi anayopata ni kupoteza urithi na hali bora aliyokuwa nayo alipokuwa kwenye mahusiano na baba yake. Luka 15:17-24 “Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia.”
Hali hiyo ya taharuki za shangwe ndiyo inayowasubiri watakatifu wa Bwana siku watakapoingia mbinguni. Mungu amewaandalia utajiri usiomithilika. 1 Petro 1:3-4 “Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.” Urithi huo unatokana na ahadi ya Mungu kwa Abrahamu. Mwanzo 15:4 “Nalo neno la Bwana likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi.” Abrahamu aliahidiwa mbaraka katika uzao wake kupitia ahadi iliyotolewa kwake. Wagalatia 4:23 “Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa mwungwana kwa ahadi.” Wagalatia 4:28 Basi, ndugu zangu, kama Isaka sisi tu watoto wa ahadi. Sifa ya kuwa watoto wa ahadi tunaipata kupitia kwa Kristo mwenyewe alipotuzaa mara ya pili.
Sisi sote ni watoto wa Adamu ambaye alihukumiwa kifo lakini tunapomgeukia Yesu tunapokea asili nyingine inayotuingiza katika urithi wa uzima wa milele. Yohana 17:24 “Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu.” Ufunuo 3:21 “Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.” Kwa nini Yesu alifanyika mwanadamu? Ili arejeshe sifa inayomstahili mzaliwa wa kwanza aliyoipoteza Adamu. Warumi 8:29 “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.”
Adamu alipoteza haki ya mzaliwa wa kwanza kwa kuyatii mapenzi ya mwili. Kristo aliyefanyika mwanadamu alitii mapenzi ya Mungu na kuutiisha mwili na hivyo kukomboa nafasi ya mzaliwa wa kwanza aliyoipoteza adamu. Leo wale wanaomwamini Yesu wanapokea haki ya mzaliwa wa kwanza aliyoirejesha Yesu na wanakuwa warithi wa ile ahadi ambayo mwanzo iliahidiwa kwa Isaka na kutimia kwa Yesu Kristo.
Mzaliwa wa kwanza alikuwa na haki gani? Mwanzo 49:3 “Reubeni, u mzaliwa wangu wa kwanza, Nguvu zangu, na malimbuko ya uwezo wangu. Umewapita wengine kwa ukuu na kwa nguvu.” Zaburi 89:27 “Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza, Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.” Danieli 7:25-27 “Naye atanena maneno kinyume chake Aliye juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati. Lakini hukumu itawekwa, nao watamwondolea mamlaka yake, kuipoteza na kuiangamiza, hata milele. Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; ufalme wake ni ufalme wa milele, na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii.”
Waliokombolewa wataanza kazi yao waliyowekewa tangu kuumbwa kwa dunia. “Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika, basi si zaidi sana mambo ya maisha haya?” (1 Wakorintho 6:3) Waliokombolewa wataanza kazi ya kupitia hukumu za waliokosa nafasi ya kuokolewa. Kazi hii itahusisha malaika waovu walioacha nafasi zao na kuasi utawala wa Mungu. “Na malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu, amewaweka katika vifungo vya milele chini ya giza kwa hukumu ya siku ile kuu.” (Yuda 1:6). Itawahusu wanadamu wasiomjua Mungu na waliokataa kuitii injili ya milele. “Katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu.” (2 Wathesalonike)
Kazi hii ya hukumu ni hatua ya mwanzo ya Yesu ya kutimiza ahadi aliyowaahidia wakati wa kampeni akiwa hapa duniani. “Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.” (Ufunuo 3:21) Hii itakuwa kama semina elekezi itakayodumu kwa muda wa miaka alfu moja (karne moja) – kipindi ambacho waliokombolewa wenye sifa ya kuwa wazaliwa wa kwanza watapewa uwezo wa kiutawala usio wa kawaida. “Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi, mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika.” (Waebrania 12:22-23).
Ndugu msomaji nawe waweza kuwa katika kundi hili ukitaka. Kwa msaada zaidi wasiliana name kwa simu namba 0764600362 au pastorletta@yahoo.com Mungu AKUBARIKI SANA

****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***
Categories:

0 comments:

Post a Comment

SIKILIZA NA DOWNLOAD WIMBO "KIFO" TOKA KWA PADACK

MAHUBIRI YA USHINDI HATIMAYE 2017 HAYA HAPA