Monday, August 22, 2016

Mathayo 12:31 "Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa."

Neno KUFURU lina maana ya; Tukana, kudhihaki, kudharau, kunena mabaya juu ya Wema, kupuuza n.k. Yesu aliwaambia mafarisayo maneno hayo, kutokana na msimamo wao wa Kiroho, wa kukataa makusudi kuamini kazi ya Yesu Kristo.

Kumkufuru Roho mtakatifu ni kitendo cha kumkataa Roho mtakatifu na Kazi yake. Roho mtakatifu ndiye anafanya kazi ya Kutufunulia Nuru au Kweli ya Mungu, anatuvuta tuiamini Kweli, anatushawishi tutubu dhambi na anatuongoza tutende Mapenzi ya Mungu.

Kitendo cha kumkataa Roho mtakatifu na kumdharau, ni kujifungia mlango wa kutoifikia TOBA, na kuendelea katika Dhambi hadi mauti. Mafarisayo walifikia kiwango hicho cha kufanya Uadui na Roho mtakatifu, walikaza mioyo hadi wakamsulubisha Mwana wa Mungu.

Mtume Paulo anasema    "Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa Ile Kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi; bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao WAPINGAO. Waebrania 10:26-27, pia soma; Waebrania 6:4-6. Hivyo kufanya Dhambi kusudi, na kukataa ushawishi wa Roho mtakatifu wa kuiachilia dhambi hiyo ni KUMKUFURU ROHO MTAKATIFU.

Hatua ya Mwisho baada ya makufuru, ni Roho mtakatifu kuacha kukushawishi, anakuwa amezimishwa, hofu ya Dhambi inapotea, Dhambi inakuwa kitu cha kawaida, inakuwa ni kitu cha kawaida ... Uzinifu, kuishi na mume au mke wa mtu, masengenyo, uongo, visasi, wizi, ulevi, upendeleo, wivu n.k. inakuwa ni sehemu ya maisha. Roho mtakatifu anakuwa amezimishwa - 1Wakorintho 5:19.

Dalili za juu za kumkufuru Roho mtakatifu ni, kuuchukia ukweli na kutopenda kuusikia ukweli, na  kutafuta kila njia za kubaki katika Dhambi fulani bila kiwa na mpango wa kuiacha. Mafarisayo walifikia hapo ... wakaanza kutunga njama za kumuua Masihi, na kumwita ana Pepo wa Beelzeburi, na hatimaye kumsulubisha. Kwa namna mbalimbali, wengi leo ni Makristo kwa Jina, lakini ndai yao wanampinga Kristo na Kumsukumia mbali Roho mtakatifu, anapowashawishi waache DHAMBI.

Wito: Kabla kengele za mauti hazijagonga, Mungu anatualika tena kupitia somo hili, kusiwe na mtu atakaye mkufuru Roho mtakatifu na kupotea milele. Neema ya Yesu yatosha kumtoa kila mmoja katika Dhambi na kumuweka huru.

NAWATAKIA SIKU NJEMA YENYE BARAKA TELE

Na: Ev. Eliezer Mwangosi  - 0767 211 299.

Utabarikiwa ikiwapelekea wengine ujumbe huu.



****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***

0 comments:

Post a Comment

SIKILIZA NA DOWNLOAD WIMBO "KIFO" TOKA KWA PADACK

MAHUBIRI YA USHINDI HATIMAYE 2017 HAYA HAPA