Saturday, December 31, 2016


(Ujumbe huu ni kwa wenye hekima ya kutafakari)

Mathayo 1:21 “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu watu wake na dhambi zao”.

Kila nikijaribu kutafakari  tangazo hili la kuzaliwa kwa Yesu nikilinganisha na mambo yanayotendeka katika sherehe ya krismasi kwa walio wengi, ni matendo kinzani. Asilimia kubwa ya watu wanasherekea kimwili, ndio siku ya kukidhi mahitaji ya mwili zaidi kuliko hitaji la Roho mtakatifu kubadilisha tabia za watu, sawa na Mpango wa Mungu.

Japo tarehe 25 Desemba imekuwa siku maarufu ambayo hata wasio enda makanisani kwa mwaka mzima, wanajitahidi angalau kuhudhuria misa mojawapo, lakini tunashuhudia uovu mwingi ukitendeka, ukiwemo, ulevi, uasherati, uzinifu, maukumbi ya starehe kujaa, nyumba za wageni kujaa, fukwe za bahari zinafurika, vijana kwa wakubwa wakiwa wamejaa mihemko ya kila namna, wakitamani kuonja kila kitu, ndio siku ambayo ndoa nyingi zinajeruhiwa, bila kusahau wapenzi kusalitiana. 

Hebu kila mmoja ajiulize swali na kutafakari; Je ni kweli katika siku hiyo Yesu alizaliwa ndani yake na kukomesha kila namna ya UOVU? au ndio virusi vya dhambi vilichochewa? Jiulize ulifanya nini siku ile, uliwaza nini, na Mazungumzo yako je? Ni mihemko ya mwili na nafsi ilifaidi kwa ulevi, ulafi, mahaba, minenguo n.k. au uliongeza viwango vya Ucha Mungu?  
Siku hiyo kiuhalisia, wengi mwili unakuwa kwenye ibada, lakini mawazo yanakuwa kwenye magudulia ya pilau, makreti ya vinywaji, mialiko na miadi ya mahusiano na mapenzi, huku wakiomba ibada iishe haraka, simu zinakuwa online muda wote wakiperuzi maneno ya kimahaba ya wapenzi wao na mialiko n.k. Hayo ndiyo baadhi ya mishale ya adui shetani akiwajeruhi wengi kupitia sherehe hizi za kimwili badala ya watu kuokolewa.
Ni ukweli usiopingika kwamba sherehe hii ya Krismasi ya kila mwaka 25 desemba, haijawahi kusherekewa na kanisa la kwanza, yani Kristo mwenyewe, mitume, na wakristo waliofuata, hadi ilipopita zaidi ya miaka 300 AD, sherehe hii ilipoingizwa huko Rumi kwa lengo la kuweka mapatano (Compromise), kati ya desturi za wapagani wa Rumi waliokuwa wakisherekea kuzaliwa kwa mwana wa mungu Jua, wakipingana na wakristo waliokuwa wamepokea Injili ya kweli ya Kristo huko ulaya. Lengo kubwa lilikuwa ni kuwafanya wapagani waukubali Ukristo, kwa kuruhusu kuingia na desturi zao na kuondoa mateso ya wakristo yaliyosababishwa na tofauti hizi za kiibada. 
Japo sherehe hiyo kwa asili sio ya kikristo, na kwamba Mungu alikaa kimya bila kuweka adhimisho la kishere la kuzaliwa Yesu kama ilivyo leo, ikiwa na maana ya Kristo kuzaliwa kila siku mioyoni mwa wanadamu wanaompokea, bado wale wanosherekea wanapaswa kujua kusudi la Yesu kuzaliwa, ili badala ya mwili na nafsi kufaidika, roho ipate badiliko la kudumu, au laa wengi watakuwa wanatimiza kusudi la adui la kuweka maadhimisho na sherehe kinzani na Mpango wa mungu wa Ukombzi.
MUNGU WABARIKI WOTE MNAPOTAFAKARI JUU YA WOKOVU HALISI UPATIKANAO KATIKA YESU KRISTO NA KUAMUA KUSIMAMA IMARA.
Na: Ev. Eliezer Mwangosi  
Simu: 0767 210 299, Whatsapp: 0766 992 265 – Kwa wanaohitaji ushauri, Maswali na Maombi.



****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***
Categories: ,

0 comments:

Post a Comment

SIKILIZA NA DOWNLOAD WIMBO "KIFO" TOKA KWA PADACK

MAHUBIRI YA USHINDI HATIMAYE 2017 HAYA HAPA