Friday, February 03, 2017



Matendo ya mitume 7:9-10 "Wale wazee wetu wakimwonea wivu Yusufu, wakamwuuza aende misri. Mungu akawa pamoja naye, akamtoa katika dhiki zake zote, akampa fadhili na hekima mbele ya farao, mfalme wa Misri; naye akamfanya awe mtawala juu ya misri na nyumba yake yote".

Ni jambo la kawaida kushuhudia baadhi ya watu wakipitia changamoto zinazosababishwa na watu wenye tabia ya WIVU, kama Yusufu alivyofanyiwa na ndugu zake. Wivu ni tabia chafu ya shetani, inayomfanya mtu ajisikie vibaya juu ya mafanikio ya mtu mwingine, ni hali ya mtu kuumia moyoni kwa mafanikio ya wengine.

Dhambi ya wivu ni mshale wenye sumu anaotumia shetani kuwatesa wengi, tabia ya wivu huambatana na masengenyo, kuzua uongo, maneno ya hila, kuteta, kubeza, kuchonganisha, kwa nje wanaweza kuonekana ni marafiki na wanakupenda, kumbe ndani kunafuka moto. Kila wakati wanakuwa na mawazo hasi juu ya wengine na kuwatakia kushindwa.

Nilishuhudia mama mmoja aliyesababisha binti kuachwa na mchumba, kwa kumtungia na kueneza sifa mbaya, akishuhudia uongo kuwa si mwaminifu, na ndivyo hata ndoa nyingi zinavyoyumba kama sio kusambaratishwa, bila kusahau wivu maofisini, mashuleni, Makanisani, kwenye biashara, hata mtu akinunua nguo nzuri, utashangaa wanapokutana wanamsifia, akiwapa kisogo tu wanabinua midomo ya kubeza. Maneno ya kusemana vibaya hayaishi kwa sababu ya tabia hii ya WIVU.

ATHARI: Wale wote wenye tanzi hii ya wivu, wanaokerwa na mafanikio ya wengine, hawatafanikiwa, na mwisho watakufa kimwili na zaidi sana kiroho, kwa sababu wanafanya kazi ya adui shetani. Neno linasema "Kwani hasira humwua mtu mpumbavu, nao WIVU humwua mjinga" Ayubu 5:2, ndio maana waswahili wakaishia kusema "Mwenye WIVU ajinyonge".

USIOGOPE: Kwa wote wanaopitia changamoto za kuonewa wivu na watu wengine, kwa mafanikio ya aina yoyote, yawe ya kimwili au ya kiroho, kupitia neno la leo, wakumbuke kuwa Mungu yupo kwa ajili ya kuwashindia, kama Yusufu alivyotolewa katika dhiki hadi utawala, ndivyo itakavyokuwa kwa kila mmoja, atakayefanyiwa hila kwa WIVU atakavyotoka kwa ushindi mkuu. Bwana yuko upande wako, wewe ni mshindi daima .... USIOGOPE.

WEMA WA MUNGU UMZUNGUKE KILA MMOJA WETU APATE KUUSHINDA WIVU

NAWATAKIA SIKU NJEMA YENYE MAFANIKIO NA BARAKA TELE.

Na: Ev. Eliezer Mwangosi
Simu: 0767 210 299 na WhatsApp - 0766 992 265




****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***
Categories: ,

0 comments:

Post a Comment

SIKILIZA NA DOWNLOAD WIMBO "KIFO" TOKA KWA PADACK

MAHUBIRI YA USHINDI HATIMAYE 2017 HAYA HAPA