Wednesday, January 21, 2015


Simulizi hizi muhimu itakuwa inakujia kwa siku 3 yaani Jumatano,ijumaa na jumapili.
Imeandaliwa na Mch J.Kuyenga
Historia ya Kanisa la Waadventista Wasabato katika sehemu za kati,Mashariki,Kusini na magharibi mwa Tanzania.
UTANGULIZI
Injili ya milele kama inavyohubiriwa na kanisa la Waadventista Wasabato ulimwenguni,imeingia hapa Tanzania mwaka 1903 ikiletwa na wamishenari waliotokea Ujerumani.Wakati huo nchi ya Tanzania ilikuwa ni koloni la Wajerumani ikiitwa Tanganyika,hivyo ilikuwa ni rahisi kwa wamishenari wa kijerumani kuzuru Tanganyika kwa lengo la kueneza imani.
Wamishenari watatu wa kijerumani walipofika Dar Es Salaam kwa meli walisafiri hadi milima ya Upare kaskazini mwa Tanganyika kuweka kambi katika maeneo ya Pare ya kusini wilaya ya Same,tarafa ya Mamba,Kijiji cha GITI.Kutokea Giti walieneza imani katika ujrani wa Pare kusini,milimani,walielekea SUJI na pia kusini zaidi kuelekea Kihurio.Kwa kutumia masomo ya Sauti ya Unabii,imani ya Kiadventista ilianza kuenea mbali na eneo la Pare ya Kusini.
=================
Kutokea Upare wamishenari hawa walielekea kanda ya ziwa sehemu za Majita(musoma) na usukumani(Bariadi).Watu wachache waliopokea imani hii mpya waliwafundisha wengine kwa bidii wakitumia biblia,masomo ya unabii(vop) na vitabu vya dini hii na wafuasi wakalipokea neno la Mungu.
Kama matokeo ya uenezaji injili mahali mahali,kanisa la waadventista wasabato lilijengwa kule Musoma,kijiji cha Busegwe na baadaye pakawa na makao makuu ya kanisa la waadventista wasabato la Tanganyika.Kutokea hapo Busegwe huduma zote za kimishenari ziliratibiwa,kwa Tanzania yote hadi mwaka 1978 makao makuu ya kanisa hili yalipohamishiwa Njiro Hill,Arusha na uongozi uliokuwepo wakati huo.
=============================
Baada ya wamishenari wa kijerumani(wageni) kutuletea imani ya injili,waafrika wachache waliopokea walikuwa tayari kuiendeleza kwa kuieneza kama wamishenari wenyeji.Kutokea Majita na Usukumani wamishenari walienda Uganda;wakati kutokea Upareni wamishenari walienda Morogoro,Dar Es Salaam na baadaye kusini mwa Tanzania.Usimamizi wa wamishenari wote hawa ulitokea Busegwe,Musoma.
Miongoni mwa wamishenari walioanzisha kazi katika miji ya Dar Es Salaam na Morogoro kwa kutumia huduma ya uinjilisti wa Vitabu watakumbukwa sana wainjilisti wawili kutokea Upareni nao ni Ndugu Misheto Mgeni na Ndugu Yohana Lukwaro.
==========================
Huduma yao inakumbukwa kuanzia mwaka 1958.Ndugu Misheto alifanyia kazi Dar Es Salaam wakati ndugu Lukwaro alikuwa Morogoro.Kwa kutumia huduma za uinjilisti wa vitabu na huduma  ya masomo ya sauti ya unabii,wanafunzi waliongezeka na waumini pia wakaongezeka katika maeneo haya ya mashariki.Ndipo ikaonekana ni lazima uongozi uimarishwe katika maeneo ya mashariki,kusini na magharibi kwa kufungua ofisi za usimamizi wa kazi mjini Morogoro.Mwaka 1968,kulianzishwa filidi yenye makao makuu Morogoro,baada ya kutengwa Kanisa la Morogoro mjini mwaka 1967.Viongozi wake wawili waikuwa ni 1 Mch.H.Henning-Mwenyekiti na 2 Mch.Reuben Ngasani,Katibu/mhazini.Filidi hii ya ilipewa jina la T.G.F(Tanganyika General Field).Eneo la utume wa TGF lilihusisha mikoa 14 ya Tanganyika ambayo ni Kigoma,Kagera,Tabora,Singida,Dodoma,Morogoro,Pwani,Dar Es Salaam,Iringa,Mbeya,Ruvuma,Rukwa,Mtwara na Lindi,kwa kutumia majina yanayotumika leo.Viongozi hawa wawili ndio waliojenga ofisi ya filidi inayotumiwa hadi leo.Ofisi hii pia ilitumiwa kama shule kuendeshea masomo ya sauti ya unabii
..ITAENDELEA IJUMAA
****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***
Categories:

0 comments:

Post a Comment

SIKILIZA NA DOWNLOAD WIMBO "KIFO" TOKA KWA PADACK

MAHUBIRI YA USHINDI HATIMAYE 2017 HAYA HAPA