Yohana
1:12-13. "Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa
Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si
kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu".
Ni
jambo la kawaida siku hizi kuona watu wanaojiita watu wa Mungu, au
wakristo, au waislamu safi n.k. Wakiwa wanahangaika huku na kule
kutafuta msaada wa kutatua changamoto zinazowasibu. Siku hizi manabii,
mitume, wapiga lamli, mafundi na waganga wa kienyeji, wamekuwa na kauli
mbiu moja ya "Njoo upokee muujiza wako sasa". Na mwisho, wanaishia
kupata miujiza isiyo na tumaini la Uzima wa milele.
Utamkuta
mtu anadai ameokoka siku nyingi, lakini bado anasumbuliwa na nguvu za
giza, watu wanahaha, huku na kule, lakini ndio kwanza mishale ya shetani
inazidi kuwatesa kwa njia moja au nyingine. Miito ya kupata miujiza ya
uponyaji magonjwa, baraka, utajiri, kuondoa mikosi au laana, inasikika
kila kona, lakini ndio kwanza watu wanazidi kuvunjika mioyo, au
wanafanikiwa kwa muda fulani, lakini baadaye wanaishia maisha duni.
Wapendwa;
muujiza mkuu ambao kila mmoja anapaswa kuupokea leo, ni KUZALIWA MARA
YA PILI, unaotokana na kujisalimisha kwa Kristo, kuruhusu awe Bwana na
Mwokozi wetu, akitawala maisha yetu. Kuzaliwa mara ya pili ni kitendo
cha kuunganishwa naye kwa njia ya Roho mtakatifu, ni kubadilishwa tabia
au nia na matakwa yetu kufanana na mapenzi ya Mungu.
Hebu
tafakari ahadi ya Yesu - Yohana 14:23, "Yesu akajibu, akawaambia, mtu
akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi
tutakuja kwake, na kufanya makao kwake". Mungu akiwa ndani yetu, kila
kazi mbovu za shetani zinateketezwa, kila mishale inavunjika, kila
majaribu yanakuwa na milango ya kutokea. Kwa kusoma neno la Mungu
tunaitambua dhambi na kujua njia halisi ya kuokolewa kupitia kafara ya
Yesu Kristo. Soma pia - Yohana 14:20-21, 1Yohana 2:1-4, Yakobo 2:10-12.
Umizimu
na changamoto zisizoisha kwa watu wa Mungu leo, ni matokeo ya kuzuka
kwa manabii na mitume wa uongo wanao wapatia watu wokovu bandia, usiotii
neno la Mungu na Sheria zake. Utamkuta mzee wa kanisa, ana nyumba
ndogo, wengine wamepora waume au wake za watu, wauza vileo na walevi,
wazinifu, wenye mapato ya aibu, hao hawakemewi wala kuonywa, kwa sababu
ya Mafungu ya kumi makubwa wanayotoa pamoja na Sadaka za kuwategemeza
watumishi.
WITO:
Bila kujali mapito uliyopitia, fungua moyo wako sasa, mwambie Yesu
atawale moyo wako, awashe Nuru mpya inayofukuza giza, na hatimaye
kuwekwa huru na kila mizigo iliyoletwa na adui. MUUJIZA MKUU KULIKO YOTE
NI KUWA NDANI YA YESU KRISTO. Soma neno la Mungu na kuomba kila siku,
ili uukulie wokovu, bila kusahau kuwasuhudia wengine habari njema.
USHINDI NI HAKIKA.
NAWATAKIA SIKU YENYE KUJAA BARAKA ZA BWANA TUKIDUMU KUTENDA MATENDO MEMA KATIKA YEYE ATUTIAYE NGUVU. Na Ev. Eliezer Mwangosi - Simu: 0767210299 - Email:
Eliezer.mwangosi@yahoo.com
****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***
0 comments:
Post a Comment