Wednesday, June 08, 2016

 Siku moja Yesu alikutana na Nikodemu. Mtu huyu alikuwa akisumbuliwa na jambo moyoni mwake na aliamini ni Yesu tu anayeweza kumsaidia. Lakini Nikodemu alikuwa mtu mkubwa. Aliogopa watu akaja kwa Yesu usiku ili watu wasimwone. Yesu alikutana na hitaji lake na bila kupoteza muda alimwambia, “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.” (Yohana 3:3-6).
Tunapaswa kuzaliwa tena
Sisi wote tunahitaji kuzaliwa mara ya pili. Tunahitaji kubadilika. Tunahitaji kuzaliwa kwa Roho. Nia zetu zinahitaji kubadilishwa. matendo yetu yanaashiria kuwa kuna jambo linahitaji kufanyika maishani mwetu ili tuishi maisha yale ambayo Mungu aliyakusudia. tangu tulipoanguka dhambini mioyo yetu imetuongoza vibaya na kujikuta tukifanya maamuzi yasiyo sahihi. Yeremia 17:9 “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?” Mungu anataka kufanya upasuaji wa moyo wako. Anataka uweke sahihi kama umekubali huduma hiyo. Mithali 23:26 “Mwanangu, nipe moyo wako; Macho yako yapendezwe na njia zangu.” Muujiza huu ambao kwa kawaida huanzia ndani kwenye eneo la kufanyia maamuzi huhitimishwa na kitendo kinachofanyika mwilini kwa nje. Kitendo hicho kinachohitimisha operesheni ya moyo kinaitwa ubatizo.
Ubatizo ni sharti la kuokolewa
Yesu amenituma kwako ili nijifunze nawe na uelewe unachopaswa kufanya. Yesu amenituma nikupe taarifa sahihi ili zikusaidie kufanya maamuzi sahihi na ya haraka. Taarifa ya kwanza muhimu ni hii Yesu anakupenda sana. Taarifa ya pili muhimu ni hii Yesu alikununulia wokovu. Tunasoma kwenye Ufunuo 5:9 “Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa.”nabii Isaya anafafanua ununuzi kuwa ulikuwa kama wa kugomboa kitu kilichouzwa kitapeli. Isaya 52:3 “Maana Bwana asema hivi, Mliuzwa bure; nanyi mtakombolewa bila fedha.”
Kisa cha kuuzwa kwetu
Kisa cha kuuzwa kwetu ni cha kusikitisha sana. Kilifanyika pasipo sisi kufahamu. Tulipozinduka usingizini kumbe tumeshauzwa! Paulo anasema katika 1 Timotheo 2:14 “Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.” Tulihadaiwa na shetani. Lakini Mungu ni mwema akamtuma Yesu akaja kutununua tena. Gharama ya kukombolewa kwetu ni kubwa kuliko kitu chochote cha thamani unachokijua. Paulo anadokezea thamani ya malipo yetu katika 1 Petro 1:18-19 “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.”
Sharti la kunufaika na ukombozi
Ili kukombolewa kwako kukamilike unatakiwa ufanye mambo mawili muhimu. Unatakiwa uamini na kubatizwa. Marko 16:16 “Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.” Biblia haisemi abatizwaye na kuamini inasema aaminiye na kubatizwa. Ni lazima mtu atangulie kuamini kwanza halafu ndipo abatizwe. Kuamini ni kutumia akili kwa kupambanua mambo. Mathayo 28:19-20 “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Mtu asiye na uwezo wa kupambanua mambo au mwenda wazimu hawezi kuamini. Huyo Mungu atamuokoa kwa njia nyingine. Lakini waweza kujiuliza hivi imani hupatikanaje? Warumi 10:17 “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” Kila unachoamini hakikisha kimetokana na Neno la Kristo. Ukiamini mambo yaliyotungwa na wadamu imani hiyo ni bure. Mathayo 15:9 “Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.”
Shetani anachukia ubatizo
Shetani aliapa kuutokomeza ubatizo wa Biblia. Anauchukia kwa sababu unamnyang’anya watu aliowashikilia mateka. Amebuni njia za kupotosha ubatizo ili watu wasinufaike na wokovu ambao Yesu amewanunulia. Yesu hali akijua hilo na akitaka watu wasipotoshwe kirahisi aliamua yeye mwenyewe abatizwe ili kuwapa kielelezo wanadamu wote. Hakuona ubatizo kama kitu cha kujidhalilisha kama sisi tuonavyo. Hata mchungaji aliyembatiza alitaka kukataa kumbatiza lakini yeye alisisitiza abatizwe. Mathayo 3:13-17 “Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe. Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali. Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.”
Watoto wadogo hawabatizwi
Yesu alibatizwa ili kutupa kielelezo, ili kututia moyo tusiache kubatizwa. Anajua hasara tutakayoipata tukikataa kubatizwa. Anajua. Kama ulibatizwa ukiwa mtoto mdogo wewe hujabatizwa kwa sababu Yesu hakubatizwa akiwa mtoto mdogo ila alibarikiwa tu. Luka 2:21-22 “Hata zilipotumia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba. Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana.” Watoto wadogo hawahitaji kubatizwa kwa sababu hawaelewi wakifundishwa, hawaamini wakifundishwa na hawawezi kufanya maamuzi. Ubatizo ni tendo la kisheria kwa hiyo ni lazima mtu ale kiapo. Kwenye kiapo cha ubatizo ni lazima mtu aseme namkataa shetani na kazi zake zote yeye mwenyewe si kwa kusemewa. Watoto wanaobatizwa wakiwa wadogo wanaonewa. Yesu hakuagiza watoto wabatizwe. Aliagiza wabarikiwe. Marko 10:13-16 “Basi wakamletea watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia.”
Yesu hakunyunyizwa maji kichwani
Yesu alibatizwa kwenye maji mengi siyo kwa kunyunyiza kichwani. Yesu alifananisha ubatizo na maziko. Mtu anayezikwa huzikwa mwili mzima na si kiungo kimoja. Kubatizwa ni kuifia dhambi. Je kule kuacha viungo vingine vya mwili bila kuvibatiza kunaashiria nini? Unataka hivyo viungo viendelee kutenda dhambi? Warumi 6:2-6 Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi? Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake; mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena.”
Ubatizo ni mmoja
Biblia inazungumzia ubatizo wa aina moja yaani ule kuzamishwa kwenye maji mengi na unaotanguliwa na kuamini. Huo ndiyo ubatizo aliotuachia Yesu. Sisi hatupaswi kuanzisha ubatizo wetu wenyewe. Waefeso 4:5 “Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.” Wajibu wa mfuasi ni kufuata kielelezo cha kiongozi wake. Wale tunaotaka kunufaika na ukombozi ambao Yesu ametununulia inatupasa kufuata nyayo za kiongozi wetu mkuu Yesu Kristo. 1 Petro 2:21 “Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake.” Yesu ametuachia kielelezo cha ubatizo hatuna haja ya kubuni mwingine wa kwetu. Mtu anayebatizwa kwa ubatizo ulioagizwa na Biblia anaitwa mtoto wa Mungu na Roho Mtakatifu hutua juu yake ili amuongoze. Mathayo 3:16-17 Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.”
Je ungependa kusikia Mungu akisema maneno hayo juu yako. Je unapenda kuifia dhambi kwa ubatizo wa maji mengi? Je ungependa ukaliwe na Roho Mtakatifu akuongoze maishani mwako? Jiunge na mamilioni wanaojitoa ili wabatizwe kama Yesu alivyobatizwa. Ukihitaji msaada wasiliana nami kwa 0764600364. Mungu akubariki sana


****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***
Categories:

0 comments:

Post a Comment

SIKILIZA NA DOWNLOAD WIMBO "KIFO" TOKA KWA PADACK

MAHUBIRI YA USHINDI HATIMAYE 2017 HAYA HAPA