Tuesday, January 24, 2017

 Isaya 43:4-5 "Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; Kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako".


Siku moja nikiwa katika kazi ya kuhubiri Injili, nilibahatika kukutana na dada mmoja aliyekuwa amekata tamaa na kukosa matumaini katika maisha. Nilipomuambia habari za Yesu, akacheka kwa kujidharau, akidai yeye hana thamani, kwa wanadamu na kwa Mungu pia, wala hawezi kuwa na thamani tena.

Akadai kuwa yeye pale alipo ameathirika, anasumbuliwa na magonjwa kwa muda mrefu, jamii inamnyanyapaa, umri umekwenda bila kuwahi kuolewa, anatamani angalau awe na familia lakini tayari anaona imeshakuwa jioni, umri umesogea, giza linaingia. Hivyo hataki kusikia habari zozote zinazohusu maisha, anatamani afe yaishe.

Wapendwa; bila kujali unapitia hali gani, ambayo inaweza kukufanya usijione wa thamani, kwa jamii au watu unaokaa nao, iwe nyumbani au ofisini, kwa mumeo au mkeo, kwa marafiki au ndugu - Mbele za Mungu wewe ni wa thamani na bado kuna tumaini.

Mpendwa; Watu wanaweza wasikuthamini, wala kukuheshimu au kukupenda, kwa sababu yoyote ile, iwe tabia yako mbaya, au dhambi, au magonjwa, au hali ya kutojiweza kiuchumi, au maumbile yako yalivyo au kwa sababu yoyote ile, Mungu anasema: Wewe ni wa thamani, anakuheshimu na anakupenda.

Kama Mungu alivyowapenda waisraeli, wangali wakiwa waovu chini ya utumwa wa farao na hatimae kuwakoa, bila kusahau tendo la Yesu kutupenda na kuja kutukomboa kwa damu yake ya thamani, tungali ni waovu, hatuna budi kujisikia wa thamani mbele za Mungu sawasawa na ahadi zake.

Hebu kila mmoja wetu akajawe na matumaini tena katika siku ya leo, bila kujali hali unayopitia wala watu wanakuonaje, kaza macho kutazama ahadi za Mungu, yeye ataujaza moyo wako tumaini kuu na kubeba haja zako.

NAWATAKIA SIKU NJEMA YENYE KUJAA AMANI NA TUMAINI KUU.

Na: Ev. Eliezer Mwangosi - Simu: 0767 210 299, WhatsApp: 0766 992 265.




****TUMA PICHA NA VIDEO WhatsApp 0713 059 073 NA 0717 367 693***
Categories: ,

0 comments:

Post a Comment

SIKILIZA NA DOWNLOAD WIMBO "KIFO" TOKA KWA PADACK

MAHUBIRI YA USHINDI HATIMAYE 2017 HAYA HAPA